NAIBU WAZIRI UMMY AMEITAKA HALMASHAURI YA SAME KUTENGA BAJETI YA KUKABILIANA NA MAAFA YANAPOTOKEA.

NA WILLIUM PAUL, SAME.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga ameitaka halmashauri ya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kutenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na maafa yanapotokea pamoja na kuyatambua maeneo yote hatarishi.

Naibu Waziri Ummy alitoa kauli hiyo jana wakati akikabidhi msaada wa vyakula mahindi tani 3.2, ndoo 25, madumu 25, vikombe na vijiko kwa waathirika wa mafuriko wa kata za Bombo, Msindo, Mtii, Maore na Vuje wilayani Same ambapo jumla ya watu sita walifariki Dunia kwa kuangukiwa na ngema katika nyumba zao.

Alisema kuwa, kuwepo kwa bajeti hiyo kunasaidia kuwahudumia waathirika wa maafa mara moja pale yanapotokea hali ambayo itasaidia kuwarejeshea tabasamu waathirika wakati wanapoendelea kusubiria msaada kutoka serikali kuu.

Aidha pia amewaagiza halmashauri hiyo kuyatambua maeneo yote hatarishi na kuanza kuwaelimisha wananchi kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka madhara mbalimbali yanayoweza kutokea.

“Halmashauri sasa mnawajibu wa kuhakikisha katika bejeti yenu mnatenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na maafa pindi yanapotokea ili muwahi mapema na kuwasaidia wahanga kwa haraka lakini yapo maeneo ambayo ni hatarishi maafa yamekuwa yakijirudia rudia mnapaswa kuyatambua na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhama” Alisema Naibu Waziri Ummy.

Pia ameitaka halmashauri, kuandaa mipango ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na kuimarisha vifaa vya uokozi.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa, kwa sasa serikali imeshapeleka wataalam wa utafiti wa miamba katika maeneo hayo ili kufanya uchunguzi kubaini hali hali ilivyo ya miamba hiyo pamoja na kubainisha maeneo yote ambayo ni hatarishi.

Katika hatua nyingine amemuagiza Mkurugenzi wa kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha anawapelekea wananchi hao mbegu za mahindi na mpunga haraka ili kurejesha mazao ambayo yamesombwa na maji kuepukana na kuibuka kwa janga la njaa hapo badae.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema kuwa, katika mafuriko hayo watu 10 wamepata madhara ambapo kati yao watu 6 wamefariki Dunia kutokana na kuangukiwa na vifusi katika nyumba zao.

Kasilda alisema kuwa, nyumba 34 zimeharibika na hekari 260 za mazao zimeharibika pamoja na miundombinu ya barabara ambapo kwa sasa serikali inaendelea na juhudi za kurejesha mawasiliano.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, kwa sasa wameelekeza watu wote ambao wako katika maeneo hatarishi kuhama katika maeneo hayo pamoja na kuhamasisha kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua hasa katika maeneo ya mito na maeneo yenye ngema.

“Tumewaagiza wakala wa Barabara Tanroad kuhakikisha mlango wa daraja la Komwex linalounganisha kijiji cha Maore na Mheza kupanuliwa ili kuwezesha magogo na takataka za mashambani kupita kwa urahisi na kutosababisha maji kupita juu ya daraja” Alisema Kasilda.

Naye Diwani wa kata ya Maore, Rashid Juma alisema kuwa, wananchi wa kata ambazo zimesombwa na mafuriko ni wakulima ambapo mazoe yao yamepelekwa na maji na kuiomba serikali kuwasaidia kupata mbegu za mahindi na mpunga ili waweze kurejea shambani na kulima ili kupambana na baa la njaa.

“Mifereji yetu mingi imeharibiwa na mvua tunaiomba serikali itume wataalam wake kuja kurejesha mifereji yetu hii pamoja na kutupatia mbegu turejee mashambani kulipa hiki ndio kilio chetu kikubwa maana hata mkitupa chakula leo kitaishi na tutarudi kulekule kwenye kuomba lakini tukirejea mashambani tutajitegemea wenyewe” Alisema Juma. 


Related Posts