Ndege nyingine yapata ajali Canada, chanzo chatajwa

Canada. Ndege ya Shirika la Canada Express imepata ajali wakati ikitua katika uwanja wa Kimataifa wa Halifax Stanfield uliopo Nova Scotia nchini Canada.

Ajali ya ndege hiyo namba DHC-8-402, iliyokuwa ikitokea Uwanja wa St. John’s, Newfoundland kwenda Uwanja wa Halifax Stanfield nchini humo ilitokea usiku wa kuamkia Jumapili Desemba 29, 2024.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafirishaji nchini Canada, uchunguzi wa awali unaonyesha ndege hiyo ilipata changamoto katika mfumo wa gia ya kutua muda mfupi baada ya kukaribia kutua katika uwanja huo.

Msemaji wa Shirika la ndege la Canada linalomiliki ndege hiyo, Peter Fitzpatrick amesema abiria wote 73 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walitoka wakiwa salama.

Fitzpatrick amesema ndege hiyo ilishindwa kutua ipasavyo kwenye njia ya kutua na badala yake tairi yake ya kulia ilisugua sakafu na kuanza kutoa cheche jambo liloloibua taharuki kwa abiria.

Hata hivyo, Fitzpatrick amesema cheche hizo ilidhibitiwa kwa wakati kwa vikosi vya kupambana na majanga ya moto kufika eneo hilo muda mfupi na kuwanusuru abiria waliokuwemo.

Abiria aliyekuwemo ndani ya ndege hiyo ameieleza CNN kuwa Nikki Valentine alishuhudia cheche za moto upande mmoja wakati ndege hiyo ikitua.

 “Ndege ilitua ghafla tukaanza kuona cheche za moto mfululuzo upande wa kushoto kisha moto ukafuka kwa wingi kutokea madirishani,” amesema Valentine.

Ndege hiyo tayari imeshaondolewa katika uwanja huo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Shirika hilo na ndege lilitoa taarifa nwa Umma likisema hakuna abiria aliyepata madhara na kusema limashukuru Mungu kwa sababu hakuna madhara kutokana na ajali hiyo.

Uwanja huo ulifungwa baada ya dakika 90 kupita tangu kutokea kwa ajali hiyo, hata safari zilizotakiwa kufanyika katika uwanja huo ziliahirishwa kwa mujibu wa Msemaji wa Uwanja wa ndege wa Halifax nchini humo.

“Safari za ndege zetu zimesitishwa kwa muda zilizotakiwa kutua hapa zimebadilishiwa njia za kutua wakati huu ambao tunafuatilia suala hili,”

Tayari Bodi ya Usafirishaji nchini Canada imeanzaa uchunguzi wa tukio hilo na maofisa wataalam wa masuala ya anga waliwasili eneo hilo Jumapili jioni.

Tukio hilo limetoa zikiwa zimepita siku mbili baada ya ndege ya Shirika la Jeju la nchini Korea Kusini ipate hitilafu katika mfumo wa gia ya kutua na kugonga nguzo zilizoko kwenye ukingo wa uwanja Muan kisha kulipuka.

Ajali ya ndege hiyo ya Shirika la Jeju iliyotokea katika uwanja ws Muan nchini humo ilikuwa ikitokea Bangkok Thailand kwenda Muan nchini Korea Kuini.

Kutokana na ajali hiyo abiria 179 walifariki huku wahudumu wawili waliokuwa kwenye sehemu ya nyuma ya ndege hiyo wakijeruhiwa vibaya.

Taarifa za awali za uchunguzi pia zibadai chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu kwenye mfumo wa gia ya kutua wa ndege hiyo.

Related Posts

en English sw Swahili