Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limepiga marufuku uchomaji wa matairi, upangaji mawe barabarani huku likiwataka wamiliki wa baa na kumbi za starehe kuzingatia masharti ya leseni zao ikiwamo muda wa kufunga na kuepuka msongamano wa watu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 31, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo jeshi hilo limejipanga kuhakikisha Sikukuu ya Mwaka Mpya 2025 inasherehekewa kwa amani na utulivu ikiwamo katika mkesha.
Amesema upigaji wa fataki utafanyika kwa wale wenye vibali rasmi huku akiwataka wananchi kutofyatua fataki kwenye makazi ya watu.
“Katika mkesha wa mwaka mpya, Jeshi la Polisi linakataza na kutoa angalizo kwa wananchi ikiwamo kuchoma matairi, kupanga mawe barabarani pamoja na kuleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara na uharibifu wa miundombinu hiyo.
“Wamiliki wa baa na kumbi za starehe wazingatie masharti ya leseni zao zinazoonyesha muda halisi wa kufunga na kuepuka kujaza watu kupita uwezo stahiki,” inaeleza taarifa hiyo.
Kuhusu mkesha wa Mwaka Mpya, Kamanda Masejo amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha unasherehekewa kwa amani na utulivu.
“Kwa kuzingatia kwamba kutakuwa na mkesha ulioandaliwa na mkuu wa mkoa, baadhi ya barabara chache zimefungwa ili kufanikisha shamrashamra maalumu za mwisho wa mwaka mkoani hapa.
“Aidha, tunawashukuru na kuwapongeza madereva wote wanaotii na kufuata sheria za usalama barabarani mkoani hapa, tunawaomba watoe taarifa za madereva wachache wazembe wanaovunja sheria za usalama barabarani ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema.