TIMU ya kikapu ya Polisi na Stein Warriors zinaendelea kukabana koo katika nafasi mbili za juu za Ligi ya Kikapu ya Daraja la Kwanza inayoendelea katika Uwanja wa Bandari, Kurasini, Dar es Salaam.
Katika msimamo wa ligi unaonyesha Polisi inaongoza katika ligi hiyo ikiwa na pointi 26, huku Stein Warriors ikishika nafasi ya pili kwa pointi 25.
Nafasi ya polisi ilipatikana baada ya timu hiyo kuishinda PTW kwa pointi 67-39, huku Stein Warriors ikiifumua Kigamboni Heroes kwa pointi 75-49.
Katika mchezo wa Polisi na PTW, timu ya PTW ilianza kuongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 9-8, huku zile zilizofuata Polisi ikirejea na kuaongoza kwa pointi 18-9, 16-8, 25-13.
Katika mchezo huo mkali uliokuwa na ufundi mwingi Fahmi Hamadi wa Polisi aliongoza kwa kufunga pointi 19 akifuatiwa na Lawi Mwambasi aliyefunga 15.
Kwa upande wa PTW alikuwa ni Mohamed Jaffer aliyefunga pointi 10 akifuatiwa na Saidi Jumanne aliyetupia nyavuni alama nne.
Nayo Stein Warriors katika mchezo wake dhidi ya Kigamboni Heroes iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 18-6, 18-17, 16-13 na 23-13.
Baraka Lema wa Stein Warriors aliongoza kwa kufunga pointi 20, huku Charles Olomi wa Kigamboni Heroes akifunga 13.
MSIMAMO WA LIGI
TIMU PL W L PTS
Polisi 13 13 0 26
Stein Warriors 13 12 1 25
Kurasini Heat 13 10 3 23
Mbenzi Beach 13 10 3 23
Chang’ombe Boys 13 9 4 22
Christ the Kings 13 8 5 21
Kigamboni Heroes 13 8 5 21
Magone 13 8 4 20