Mtama. Rais Samia Suluhu Hassan ametekeleza ahadi yake ya kugawa miche 500,000 ya minazi kwa wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika miche hiyo, Lindi pekee imepokea miche 60,000.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo kwa maofisa kilimo kutoka wilaya sita za Mkoa wa Lindi leo Jumanne Desemba 31, 2024, Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (Tari), Dk Fredy Tairo amesema wananchi wa mikoa hiyo waliomba miche ya minazi kwa kuwa, ya awali ilikuwa ya muda mrefu na mingine kukauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kushambuliwa na wadudu.
“Hivyo, Rais Samia baada ya kusikia maombi yao, ametoa miche 500,000 ya minazi wagawiwe wananchi hawa na Mkoa wa Lindi pekee umepokea miche 60,000. Minazi mingi ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni ya asili na inaathiriwa zaidi na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Tairo.
Amesema takribani wananchi milioni 14 wanategemea nazi, lakini uzalishaji wake umepungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi na magonjwa yanayoathiri minazi.
“Kwa kawaida mnazi mmoja unaweza kuzalisha nazi 30 hadi 35 kwa mwaka, lakini ukame na mashambulizi ya wadudu vimepunguza uzalishaji huo. Hata hivyo, miche iliyotolewa sasa ina uwezo wa kuhimili ukame,” amesema Dk Tairo.
Kaimu Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Lindi, Ramadhani Khatibu amesema ukosefu wa viwanda vidogo vya kuchakata nazi umechangia kushuka kwa thamani ya zao hilo.
“Mkoa wetu hauna viwanda vidogo, jambo ambalo limeathiri uzalishaji na thamani ya nazi. Viwanda vingesaidia kuzalisha bidhaa kama mafuta na urembo kutoka vifuu. Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa kusini,” amesema Khatibu.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Nachingwea, Huruma Chiamba amesema watahakikisha wakulima wanasimamiwa ipasavyo ili kuzalisha minazi yenye tija na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
“Zao la nazi litakuwa na thamani kubwa kwa mikoa yetu ya kusini kupitia usimamizi mzuri wa wakulima na kuimarisha uzalishaji,” amesema Chiamba.
Salma Juma, mkulima kutoka Kata ya Ng’apa amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia miche ya kisasa ya minazi inayohimili ukame.
“Miche hii ya kisasa itasaidia kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima. Sisi wakazi wa Ng’apa tunategemea sana zao hili,” amesema Juma.