Rais Samia atoa salamu akiagiza udhibiti ajali za barabarani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mwaka 2024 Tanzania ilikumbwa na jinamizi la ajali za barabarani, akieleza idadi ya watu waliofariki dunia ni 1,715.

Rais Samia amesema hayo alipotoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania leo Desemba 31, 2024.

“Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715.

“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” amesema.

Amewataka Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.

Hata hivyo, amesema mwaka 2024 ulikuwa wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotoa matumaini zaidi unapoitazama kesho ya Taifa.

Amesema katika jitihada za kutekeleza majukumu yake, alifanya ziara katika baadhi ya mikoa ambako alijionea ari na hamasa ya wananchi kujiletea maendeleo.

“Kuanzia Morogoro hadi Rukwa, Mwanza hadi Ruvuma na Zanzibar, kote niliona kazi inaendelea. Serikali inatekeleza majukumu yake, wananchi wanajituma na mabadiliko yanaonekana.

Rais Samia amesema 2025 ni mwaka maalumu kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia nchini kwa kuwa utafanyika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani na kwa upande wa Zanzibar, watachagua Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

“Miongoni mwa maandalizi ya awali ya uchaguzi huo, ilikuwa ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa yaliyopelekea kurekebishwa kwa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa. Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo.

“Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki,” amesema. 

Amesema uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024 ulifanyika kwa amani na utulivu.

“Katika uchaguzi ule, kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi, kwa kupigiwa kura ya Ndiyo au Hapana. Hii imeondosha rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa, ambayo ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini,” amesema.

Amesema nchi imeendelea kusimamia utekelezaji wa falsafa ya 4R inayohimiza Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga nchi.

“Vilevile tunaendeleza uhuru wa habari unaoashiriwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni kupitia vyombo mbalimbali, hata uhuru wa kukusanyika na kujumuika,” amesema.

Katika utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Haki Jinai, amesema mwaka 2025 Serikali itakamilisha sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki jinai.

“Tutaendelea pia kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji. Hadi sasa, jumla ya wananchi 495,552 wameshanufaika na msaada wa kisheria wa kampeni ya   Mama Samia Legal Aid chini ya Wizara ya Katiba na Sheria,” amesema.

Amesema Serikali itaendeleza mchakato wa kupata maoni ya wananchi ili kukamilisha uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwezesha kuanza utekelezaji.

“Niwapongeze wananchi wote waliochangia katika mchakato huu, niwasihi tuendelee kutoa maoni yetu hadi mchakato utakapokamilika,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali itapokea ripoti ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi itakayosaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.

Rais Samia amesema mwaka 2024 ulikuwa wenye neema na mafanikio, uchumi wa nchi ukiimarika na kuwanufaisha wananchi.

Amesema kati ya Januari hadi Juni, 2024 uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

“Deni la Taifa nalo liliendelea kuwa himilivu. Mfumuko wa bei umebaki ndani ya lengo la asilimia tatu, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha,” amesema.

Amesema imeshuhudiwa ongezeko la uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), amesema kati ya Januari hadi Novemba 2024 imesajiliwa miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola bilioni 7.7 za Marekani inayotarajia kuzalisha ajira 205,000.

Kuhusu miradi ya kimkakati, amesema baadhi imeanza kutoa huduma, akikemea vitendo vya kuihujumu.

Amesema Bwawa la Julius Nyerere limeanza kuzalisha umeme na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika.

“Uzalishaji kwa sasa umefikia jumla ya megawati 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya megawati 1,888. Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unatoa huduma kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma,” amesema.

Amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikuwa linasafirisha wastani wa abiria 300,000 hadi 400,000 kwa mwaka lakini ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, zaidi ya abiria milioni 1.2 wameshasafiri na reli hiyo.

“Hapa nataka nisisitize kuwa, miradi hii ni yetu sote na imejengwa kwa kutumia rasilimali zetu. Hivyo, tunawajibika kuitunza ili itunufaishe sisi na vizazi vijavyo kesho. Vitendo vya kuhujumu miradi hii ni kulihujumu Taifa,” amesema.

Amesema miradi inayotarajiwa kuanza utekelezaji mwaka 2025 ni ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 78.9.

Mingine ni wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) chini ya Dart na mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na hoteli ya nyota nne katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Miradi hiyo amesema itatekelezwa kwa uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma.

Amesema mpaka sasa kuna miradi 74 ya ubia iliyopo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji.

Rais Samia amesema Serikali itatoa kipaumbele kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma ili kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi.

Miongoni mwa miradi amesema ni barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 80 na upanuzi wa Barabara ya Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambao umefikia asilimia 20.

Mingine ni awamu za tatu na nne za miundombinu ya barabara za mwendo kasi jijini Dar es Salaam. Pia, kuanza huduma kwenye awamu ya pili kwa njia ya Mbagala iliyokamilika.

“Mapema mwakani, tunatazamia Reli ya SGR ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma kiasi cha tani milioni moja kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita,” amesema.

Related Posts