Sababu vifo vya watoto ‘swimming pool’

Dodoma. Baada ya kuripotiwa matukio ya watoto wawili kupoteza maisha kwenye mabwawa ya kuogelea (swimming pool) katika Sikukuu ya Krismasi, angalizo limetolewa kuhusu matumizi ya mabwawa hayo ikielezwa, kuna namna yanasababisha vifo hivyo.

Katika kipindi hiki cha msimu wa mapumziko ya mwisho wa mwaka watoto wa maeneo mbalimbali ukiwamo mkoani Dodoma, wamekuwa wakiyatumia mabwawa hayo kwa burudani, hivyo tahadhari zimetakiwa kuchukuliwa ili kuepusha madhara.

Desemba 25, 2024, Mbaraka Magese alifariki dunia baada ya kuzidiwa maji alipokwenda kuogelea katika bwawa lililopo Baa ya Nzengo mjini Kahama mkoani Shinyanga.

Siku hiyo hiyo mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Miuji, Sausi Maliki (14) alifariki dunia wakati akiogelea katika bwawa la Hoteli ya African Dream jijini Dodoma.

Tukio kama hilo lilitokea pia Juni 2020, Kijiji cha Mwandege, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, baada ya Hassan Kipende (13) kufariki dunia wakati akiogelea katika bwawa la Campsite alipokwenda kusherekea Sikukuu ya Idd.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Mrakibu (SF), Rehema Menda amesema wamefanya ukaguzi na kubaini maeneo yanayohusisha watu kufa maji.

 “Maeneo ya watu kufa maji hapo tunagusa visima vya kienyeji, chemba zilizoachwa wazi bila uangalizi, mabwawa yasiyo rasmi ambayo makandarasi wametumia kuchimba vifusi na mabwawa ya kuogelea. Hoteli zenye mabwawa haya tumeshazibaini na wamefikishiwa barua,”amesema.

“Na tumewaelekeza mambo gani waweze kuzingatia ili wateja wao wanapokuwa wakipata starehe za kuogelea ama burudani hizo, waweze kuwa salama na wasitokewe na janga lolote lile,”amesema Kamanda Rehema.

Pia, amesema wamepita na gari kuwatangazia watu kuhusu kuchukua tahadhari katika maeneo yote yenye visima ikiwamo Nzuguni, Ndachi na Ipagala na Mkonze.

Aidha, wamepeleka barua makanisani na msikitini kuhusu viongozi wa kidini kuwatangazia waumini wao kuchukua tahadhari katika maeneo yao.

“Sisi tumejipanga na tayari tumekuwa na mikakati na tunaendelea kuisimamia kuhakikisha kuwa, hatupotezi watu hasa watoto ambao ndio wahanga wa hilo ambayo ni nguvu ya Taifa ya kesho,”amesema Kamanda Rehema.

Uchunguzi umebaini kuwa, kutokana na kukosekana kwa maeneo ya burudani kwa watoto jijini Dodoma, kumesababisha mabwawa hayo kutumika kama sehemu ya kustarehe nyakati za sikukuu za kidini na Mwaka Mpya.

Sehemu hizo zimekuwa zikipata watoto wengi wanaotoka maeneo tofauti ya jiji, wakienda kwa makundi kuogolea, hali inayofanya kuwepo uhitaji mkubwa wa usimamizi wa watalaamu wa kuogelea.

“Wengi wao huogelea sikukuu hadi sikukuu kutokana uwezo wa familia wanazotoka. Wanakuwa sio wazoefu wa kuogelea hivyo wanahitaji usimamizi ambao hawaupati katika mabwawa hayo,”amesema mmoja wa wazazi Jamila Athuman.

Kiwango kinachotozwa katika mabwawa hayo kwa watoto kuogelea ni kati ya Sh7,000 hadi Sh10,000 kwa kila mmoja.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa wenye hoteli mkoani Dodoma, Willington Malea amesema wamiliki wa mabwawa wanatakiwa kuwa na watu wanaojua kuogelea katika mabwawa yao.

 “Katika mabwawa yao wanatakiwa kuwa na vibao vinavyotoa maelekezo kwa kuwa, mtu kupoteza maisha ni rahisi sana. Haitakiwi aende moja kwa moja kuogelea kwenye bwawa badala yake wanapaswa kuanza kuoga maji ya baridi.”

Malea amesema hakuna tabia ya kuwauliza wanaotaka kuogelea historia ya afya zao kwa sababu wengine hawatakiwi kuogelea kuepuka madhara yanayoweza kutokana na uogeleaji.

Anatoa mfano wa watu wanaokabiliwa na magonjwa ya misuli, wenye vyuma kwenye mwili na kifafa.

 “Ikifika kama saa 11.00 jioni maji yanakuwa na ukungu chini, unakuta mtu anapiga mbizi sasa anaporuka kuna kingo katika bwawa la kuogelea hawezi kuziona anaenda kujigonga,”amesema Malea.

Amesema katika siku za sikukuu wengi wa watu wanaangalia fedha badala ya usalama wa waogeleaji kwa kuruhusu watu wengi bila kuangalia uwezo wa mabwawa yao.

“Unaweza kuingia katika bwawa ambalo  inatakiwa kuwa na watu 10, wanaingia zaidi ya watu 100 mle ndani. Sasa katika watu 100 mle ndani kuna watu wanaishiwa hewa na nguvu kwa hiyo kumzamisha mwenzake ni rahisi sana,”amesema.

 Malea amesema mabwawa ya kuogelea watoto yanatakiwa kuwa na urefu wa futi moja hadi na nusu.

Amesema wamiliki wa mabwawa wanatakiwa kuwa na majaketi ya uokozi, angalau kwa kuanzia majaketi 10 watakayovaa watu wote wanaotaka kuogelea.

Amesema kuwe na sanduku la kutoa huduma katika kila bwawa na kuwe na chombo cha kusimamia mabwawa hayo kuona kama yanakidhi vigezo.

Malea amesema pia kwa bwawa moja dogo la uwezo wa kuogelea watu 10, inatakiwa kuwe na mtaalamu mmoja wa uokozi atakayewaangalia watu wote waliomo ndani ya bwawa hilo.

Waaangalizi wa mabwawa kupimwa

Kamanda Rehema wa Zimamoto amesema mtu yeyote hapaswi kuendesha biashara ya bwawa la kuogelea bila kuwa na mtaalamu ambaye ni mbobezi wa shughuli za kuzamia kwenye maji na hapaswi kuwa mmoja.

 Amesema ukaguzi waliofanya katika mabwawa hayo wamegundua baadhi yana waangalizi wawili na mengine mmoja lakini kwa utaratibu wanapaswa kuwa waangalizi wawili ili wapishane, hivyo kufanya uwepo wa uangalizi muda wote.

“Isipokuwa tutakachokifanya ni kuwapima hawa watu kwa sababu ndio dhamana ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya kuwapima wasimamizi wa mabwawa haya, tuone kukidhi kwao vigezo. Hivi karibuni tutalifanya hilo hapo Chinangali. Tunataka kujiridhisha,”amesema.

Amesema shughuli hizo za kuwapima, zimekuwa zikifanyika mara kwa mara kwa kuwa baadhi ya wamiliki, huajiri watu kwa muda mfupi na kuwaondoa.

Kamanda Rehema amesema mbali na waangalizi, mabwawa hayo yanatakiwa kulindwa vizuizi vitakavyofanya kutokuwepo kwa urahisi wa watoto kuwatoroka waangalizi wao.

 Amesema pia, wamiliki wa mabwawa hayo wanatakiwa kufunga kamera ili wafuatilie wateja wao wanapokuwa wakiogelea.

Related Posts