Sultani wa mwisho wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah, afariki dunia

Dar es Salaam. Jamshid bin Abdullah, aliyekuwa sultani wa mwisho wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964, amefariki dunia nchini Oman akiwa na umri wa miaka 95. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Jamshid aliyefariki dunia jioni ya Jumatatu, Desemba 30, 2024, akiwa hospitali kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya muda mrefu na uzee, anatarajiwa kuzikwa leo, Jumanne, katika makaburi ya kifalme jijini Muscat, Oman.

Jamshid alizaliwa Zanzibar, Septemba 16, 1929 na alipata elimu ya msingi visiwani humo kabla ya kuendelea na masomo nchini Misri na baadaye Uingereza, alikohudumu kwa miaka miwili katika Jeshi la Wanamaji la Uingereza.

Alirithi kiti cha usultani Julai mosi, 1963 baada ya kifo cha baba yake, Sultani Abdullah bin Khalifa.

Uongozi wake ulidumu kwa miezi sita tu, kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, yaliyomaliza utawala wa kifalme visiwani Zanzibar.

Baada ya kupinduliwa, Jamshid alikimbilia Oman, lakini alikosa hifadhi nchini humo na hatimaye akaelekea Uingereza, alikoishi uhamishoni kwa takribani miaka 56 katika Mji wa Portsmouth.

Uhamishoni na maisha ya faragha

Kwa muda wote aliokuwa Uingereza, Jamshid aliishi maisha ya faragha, hata baadhi ya majirani zake hawakujua utambulisho wake. Mwandishi Ned Donovan aliyefuatilia maisha ya Sultani huyo anasema: “Sikupata mkazi hata mmoja ambaye alifahamu uwepo wake; hakuzungumza na vyombo vya habari na aliishi maisha ya kimya.”

Maombi yake ya kuruhusiwa kurejea Oman yalikataliwa mara kadhaa, lakini mwaka 2020, aliruhusiwa na Serikali ya Oman kuishi nchini humo kama mwanafamilia wa kifalme lakini si kama sultani.

Urithi wa utawala wa kisultani

Jamshid alikuwa sultani wa mwisho kati ya masultani 13 waliotawala Zanzibar, kuanzia Sayyid Said aliyehamisha makao makuu ya kifalme kutoka Oman hadi Zanzibar mwaka 1840.

Baada ya kifo cha Sayyid Said mwaka 1856, dola lake liligawanywa kati ya wanawe Majid (Sultani wa Zanzibar) na Thuwain (Sultani wa Oman).

Japo Jamshid hakurejea tena Zanzibar, Rais wa zamani wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, aliwahi kumpa ruhusa ya kurejea kama raia wa kawaida.

Hata hivyo, hakuona haja ya kufanya hivyo. Kifo chake kinahitimisha sura muhimu ya historia ya Zanzibar na utawala wa kifalme uliomalizika zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Related Posts