Tutayakumbuka haya mwaka 2024 katika elimu

Mwaka 2024 unatamatika leo ukiacha kumbukumbu muhimu za matukio kadhaa ya elimu yanayoufanya kuwa mwaka wa kipekee katika historia ya sekta ya elimu nchini.

2024 ndio mwaka ambao pamoja na mengineyo Taifa limeshuhudia kuanza kwa utekelezaji wa mtalaa mpya wa elimu ya amali kwa baadhi ya shule za sekondari.

Oktoba 10 mwaka 2023, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aligusia kwa nini Serikali imeanzisha elimu ya amali nchini.

Alisema lengo la Serikali ni kutaka kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambapo watakapomaliza wawe na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa, hivyo sekta binafsi kama wadau wajitokeze kwa ajili ya kutimiza lengo hilo la Serikali.

“Kwenye elimu hii ya amali tutakuwa na michezo, kilimo pamoja na ufundi ambapo mtoto atakapomaliza kusoma atapata na cheti chake alichosomea hivyo nawaomba kama kuna mtu ana uwezo wa kutoa elimu hii awasiliane na Serikali na sisi tutaboresha mazingira yake,” alisema Profesa Mkenda alipokuwa akizipigia chapuo shule binafsi kujikita kuomba fursa ya kufundisha elimu hiyo.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, mkondo wa elimu ya amali kwa mwaka huu umeanza kutekelezwa katika shule 96 ambapo 68 ni za binafsi na 28 za Serikali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Louisulie anasema watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wanasoma lakini elimu wanayopata haiwasaidii, hivyo mtalaa wa amali anauona kama mkakati sahihi wa kuwapatia wanafunzi ujuzi.

“Mtu fulani akimaliza ngazi fulani ya elimu aweze kufanya kitu, sio mtu asubiri asome chuo kikuu ndio awe na ujuzi.Elimu ya amali haina mjadala kwa kuwa ina umuhimu wake kwa sababu kazi yake ni kuwapa watu ujuzi. Sasa ujuzi wa kupika, chochote kinachofanyika duniani lazima watu wake wawe na ujuzi,’anasema.

Hata hivyo, anasema utekelezaji wake hautakosa changamoto anazosema wahusika hawana budi kuzibadilisha na kuwa fursa.

Rais Samia Suluhu Hassan, ndiye aliyeanza kuchokoza mjadala wa kitaifa kwa kuagiza kufanyike mapinduzi ya mfumo wa elimu nchini na hatimaye watendaji wake kuingia kazini na kufanya maboresho ya mtalaa wa elimu ya msingi na sekondari.

Alipohutubia Bunge mwaka 2021, Rais , aliweka bayana dhamira ya Serikali yake ya kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na kufanya mabadiliko ya mitalaa iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi kulingana na mahitaji ya soko kitaifa, kikanda na kimataifa

Akitoa maoni yake kuhusu mtalaa mpya, mwanachama wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (TAPIE), Okoka Mwapuja anasema haujafanikiwa kwa asilimia 100.

Anasema wanafunzi walioanza mitalaa mipya, mwakani wanaingia darasa la nne lakini hajaona kama walimu wamejiandaa kwa darasa la nne na hivyo walihitaji kupewa semina na mafunzo mbalimbali.

“Ninaona kuwa bado tuna changamoto katika mtalaa mpya hata performance (matokeo) ya watoto haijafikia kiwango ambacho hivi sasa wana enjoy (wanafurahia) ingawaje ni kitu kizuri kwa sababu mtalaa mpya unaelekeza wagundue wenyewe, wajifunze wenyewe badala ya kukariri,”anasema.

Anasema kuwa wawezeshaji ambao wanapeleka maarifa hayo kwa wanafunzi, bado hawajaiva vizuri, akisema pengine likizo ya Desemba ilipaswa kutumika katika semina za maboresho ya mtaalaa huo.

Anasema walimu walifanyiwa semina kabla ya kuanza kwa mitalaa hiyo , lakini zilikuwa ni za muda mfupi na za haraka.

Machi 08, 2024, Profesa Adolf Mkenda alitangaza kuwa wanafunzi wanaosoma darasa la tatu mwaka huu, watamaliza elimu ya msingi baada ya miaka sita ikiwa ni utekelezaji wa sera ya elimu iliyofanyiwa mapitio mwaka 2023.

Machi, 21,2024, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohammed Mchengerwa, alitangaza tahususi mpya kwa wanafunzi wa kidato cha tano, lengo ni kuendelea na utekelezaji wa mapitio ya sera ya elimu.

Alifafanua kuwa utekelezaji huo utahusisha uanzishaji wa tahasusi mpya 49 kutoka 16 zilizokuwepo awali na hivyo kufanya jumla ya tahususi 65 na kwamba zingeanza kutekelezwa Julai mwaka 2024.

“Tahasusi hizo mpya zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 zipo katika makundi saba ambayo ni tahasusi sayansi ya jamii, lugha, tahasusi za masomo ya biashara, tahasusi za sayansi, tahasusi za michezo, tahasusi za Sanaa pamoja na tahasusi za elimu ya dini,”alisema.

Suala la kuanzisha tahasusi hizo mpya lilileta mjadala mkubwa kwa wadau wa elimu wakihoji utayari wa Serikali kuwahudumia wanafunzi watakaochagua tahasusi 65, lakini Mchengerwa alilitea kuwa Serikali imejipanga kibajeti, walimu na miundombinu.

Hata hivyo, Julai 26, 2024 alijitokeza Profesa Mkenda akisitisha utekelezaji wa baadhi ya tahasusi kwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2024/25, kutokana na changamoto za kiufundi ikiwemo kuchelewa kuchapishwa kwa nakala ngumu za vitabu.

Kuhusu ongezeko la tahususi kutoka 16 kwenda 65, Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo anasema kimsingi Tanzania ilichelewa sana kuanza mpango huo.

“Kumwambia mtoto lazima tahasusi moja kama vile HKL awe na ufaulu kwa masomo yote, ni kama tulikuwa tunawaonea hawa watoto. Kuanzishwa kwa mpango huu kutatoa mwanya kwa watu wengine kuonyesha vipaji vyao katika sehemu ambayo ana uwezo zaidi kuliko kulazimishwa,”anasema.

Anasema awali kabla ya kuongezwa kwa tahasusi hizo, wanafunzi walifungwa kusoma masomo maalumu tofauti na sasa wana machaguo mengi zaidi.

“Ilifika mahali kama tuli-focus (tuliegemea) katika kukodisha akili (ajira), kwa nini tusiache uhuru watu wawe huru katika kufanya kile kinachowezekana. Kuanzishwa kwa tahasusi hizi ina maana ni kuruhusu bongo za watu ziweze kuzunguka,”anasema.

Anasema hata kama kutakuwa na changamoto zitatatuliwa zitakapojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango huo.

Kwa upande wake, Mwalimu Job Mwakalambo anasema kutokana na changamoto za kidunia ndio maana Serikali imeamua kuongeza tahasusi kutoka 16 zilizokuwepo awali.

“Mimi nimesoma masomo ya sayansi sekondari lakini waliosoma Kifaransa wote walifaulu…Lakini wakati ule lugha bado ilifungwa, ilikuwa usome Kifaransa au Kingereza lakini sasa kuna Kiarabu, kuna atakayechagua tahususi ya michezo. Sasa inatufanya kuongeza uwanda mpana wa kuchagua,”anasema.

Hata hivyo, anasema changamoto hazikosekani linapoanzishwa jambo, lakini kwa yeye Serikali haijawahi kufanya uamuzi wa ovyo. Anatoa mfano wakati shule za kata zilipoanzishwa watu waliziita shule za yeboyebo, lakini hivi leo zimekuwa mkombozi mkubwa kwa kuchukua wanafunzi wengi nchini.

Anasema shule hizo hazikuwa na walimu wa kufundisha lakini Serikali ilifanya uamuzi wa kuwapeleka watu kusoma miezi mitatu (walijulikana kama voda fasta), kisha kwenda kufundisha shuleni.

Hata hivyo, mwaka huu umeacha kumbukumbu kwa kujitokeza kwa matukio ya kuhuzunisha kwenye maeneo tofauti ikiwemo ajali za mabasi ya wanafunzi zilizosababisha vifo na majeruhi.

Miongoni mwa ajali hizo ni ile iliyotokea Agosti 31,2024, ambapo wanafunzi watatu na dereva walifariki dunia huku wengine 30 wakijeruhiwa kwenye ajali ya gari wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari dogo aina ya coaster lililokuwa limebeba wanafunzi hao, kugongana uso kwa uso na gari la mizigo aina ya Scania.

Ukiondoa ajali hiyo, suala la kupotea kwa mwanafunzi wakati yeye na wenzake wakiwa katika ziara ya mafunzo, liliutia doa mwaka.

Tukio hilo lilitokea Septemba 14,2024 ambapo mwanafunzi huyo wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara wilayani Babati Mkoani wa Manyara, Joel Johannes (14) alipopotea katika Mlima Kwaraa walikokwenda kwa ziara ya masomo iliyowahusisha wanafunzi 103.

Hata hivyo, baada ya jitihada za Serikali na shule aliyokuwa akisoma na wazazi, Joel alipatikana Oktoba 9,2024 akiwa amedhohofu.

Mzazi, Stella Mwakalinga anasema mabasi mengi ya kusafiria wanafunzi hayafanyiwi matengenezo ya mara kwa mara, jambo ambalo kwa maoni yake linaweza kuwa linachangia ajali.

“Serikali iweke sheria kali za kuwabana wamiliki wa shule kuhakikisha kuwa mabasi yanayotumika kuwasafirishia wanafunzi, yanakuwa na ubora na kukaguliwa mara kwa mara kuhakikisha hayana ubovu unaoweza kuleta madhara,”anasema.

Anasema pia madereva wanaoendesha magari ya wanafunzi wapewe mafunzo ya mara kwa mara, kuhusu utambuzi wa magari ili inapotokea changamoto waweze kubaini mapema.

Mzazi mwingine, Ally Yusuf anasema tukio la la mwanafunzi kupotea mlimani lilijaa uzembe kwa kutokuwa na walimu wengi wa kuwasimamia kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

“Ni vyema ziara hizi zikapata kibali kutoka ofisi ya elimu na halmashauri ili waweze kuangalia usalama wakiwa kwenye ziara hizo. Hii itasaidia kusiwepo kwa uzembe wa usimamizi wa watoto,”anasema.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts

en English sw Swahili