Songwe. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wananchi kujiepusha kujiandikisha mara mbili au kutoa taarifa za uongo wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, kwa kuwa ni kosa kisheria linaloweza kusababisha kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili jela au faini ya kati ya Sh100,000 na Sh300,000.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumanne Desemba 31, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Grayson Orcado alipozungumza kwenye mkutano na wadau wa uchaguzi.
Mkutano huo ulikuwa ukizungumzia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nselewa, wilayani Mbozi.
Grayson amesema kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa chini ya kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024.
Amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kufika katika vituo vya kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwa uaminifu na kuepuka kutoa taarifa za uongo.
Katika hatua nyingine, Grayson amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Uhamiaji, kushirikiana na wananchi kuhakikisha raia wasio na sifa hawajiandikishi kwenye daftari hilo.
Amesema Mkoa wa Songwe kutokana na kuwa mpakani, unahitaji usimamizi makini wa Jeshi la Uhamiaji ili kuzuia raia wasio na sifa kushiriki shughuli hiyo.
Aidha, amewataka viongozi wa dini kutojihusisha moja kwa moja na siasa badala yake kutumia madhabahu na mimbari kuhamasisha waumini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kuboresha taarifa zao.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa, Saida Mohammed amesema wapigakura wapya 5,586,433 wanatarajiwa kuandikishwa, sawa na asilimia 18.7 ya wapigakura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji wa mwaka 2019/20.
Aidha, amesema wapigakura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao, huku wapigakura 594,494 wakitarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa.
“Baada ya uboreshaji, daftari linatarajiwa kuwa na wapigakura 34,746,638,” amesema.
Kwa Mkoa wa Songwe, tume inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 110,803, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapigakura 619,703 waliopo kwenye daftari, hivyo kufanya idadi ya wapiga kura kufikia 730,506.
Saida amesema mpaka sasa wananchi wa mikoa 19 ya Tanzania Bara na Zanzibar wameandikishwa tangu ilipozinduliwa rasmi mkoani Kigoma Julai 20, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kiongozi wa Mila wa Wilaya ya Mbozi, Sibhelwa Nzuda amesema kazi hiyo ni muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao na kujiandikisha.
“Suala hili ni la kitaifa na linahitaji uzalendo wa hali ya juu. Kila mwananchi mwenye sifa anapaswa kujiandikisha ili kushiriki katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani mwaka 2025,” amesema Chifu Nzuda.
Uandikishaji katika Mkoa wa Songwe unatarajiwa kuanza Januari 12, 2025 na kuhitimishwa Januari 18, 2025.