WAKATI kikosi cha Simba kikielekea Tunisia alfajiri ya leo kuifuata CS Sfaxien, kiungo wa timu hiyo ambaye pia ni nahodha msaidizi, Fabrice Ngoma ametuma ujumbe, huku akitoa ujanja wanaopaswa kuutumia ili kufanya kitu tofauti.
Hiyo ni kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A utakaochezwa Jumapili, wiki hii, Tunisia ambapo Simba inahitaji ushindi au sare kujitengenezea nafasi ya kufuzu robo fainali. Ngoma amewataka wenzake kupambana bila kujali, ilimradi ushindi upatikane.
“Tunahitaji ushindi kwenye mechi ijayo. Tulifanya makosa madogo kwenye mechi ya mwisho ugenini kule Algeria, lakini tunataka kwenda kujisahihisha,” alisema Ngoma ambaye amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza cha Simba.
“Hii ni mechi ngumu na muhimu ambayo kama tutashinda tutazidi kusogeza hesabu sawa kwenda robo fainali. Hii ni mechi ambayo ipo kwetu wachezaji kwenda kuilinda heshima ya klabu yetu kubwa.”
Ngoma alisema baada ya kuwa na mwendelezo mzuri katika ligi, hali hiyo wanatakiwa kuihamishia kimataifa kwani wamekuwa hawana matokeo mazuri mechi za ugenini kutokana na kupoteza moja dhidi ya CS Constantine (2-0), lakini mbili za nyumbani wakishinda dhidi ya Bravos (1-0) na CS Sfaxien (2-1).
Awali, hatua ya mtoano ugenini dhidi ya Al Ahli Tripoli walitoka 0-0 wakashinda nyumbani 3-1 na kufuzu makundi.
Katika Kundi A, Simba ina pointi sita sawa na CS Constantine na Bravos, huku CS Sfaxien haina pointi baada ya timu zote kucheza mechi tatu. Kuhusu nafasi yake ndani ya Simba, Ngoma alisema: “Hapa kila mtu ana nafasi ya kucheza na kuisaidia timu, unaweza kuona leo nimefunga, lakini kesho kila mtu atafurahi kuona mwingine anafunga. Kitu kinachotupa faraja kubwa ni ushindi wa timu haijalishi nani amefanya hivyo.
“Hatuna nafasi ya kuangalia rekodi ya mtu mmoja unaona mashabiki wao wanataka ushindi, viongozi wanataka ushindi, makocha na hata wachezaji tunataka hilo. Kitu muhimu ni ubingwa.”
Katika misimu sita, Simba imefuzu robo fainali mara tano mashindano ya klabu CAF.