AKILI ZA KIJIWENI: Sio ajabu Morrison kusajiliwa KenGold

UKIHISI usajili uliofanywa na KenGold kumnasa winga wa zamani wa Yanga na Simba, Bernard Morrison kuwa ni jambo la kushangaza basi wewe amua tu kuachana na soka la Bongo.

Hakuna aliyeshangaa hapa  maskani kwa vile maisha ya Tanzania ni matamu na watu wengi wakija hapa kutoka katika nchi zao hasa za Kiafrika huwa wanatamani kubaki Bongo kwa muda mrefu.

Jambo kubwa ambalo linashawishi wageni wengi wawe na mapenzi makubwa na Tanzania ni amani na utulivu tulionao unaofanya kila mtu ajisikie yupo nyumbani na aishi bila bughudha yoyote ikiwa anafuata sheria na taratibu za nchi.

Asikuambie mtu kuna nchi raia hapati hata nafasi ya kutembea mtaani katika mizunguko ya kawaida, sasa anapokuja Bongo kisha akaachwa ajiachie bila kusumbuliwa huwezi kumtoa kirahisi hapa Tanzania huyo mtu.

Tanzania pia ukiwa staa hasa wa soka, maisha yanakuwa rahisi sana kwako na unapendwa na wengi hivyo sio rahisi kuteseka na maisha kulinganisha na nchi nyingine ambazo kila mtu yuko na habari zake na kama huna basi huna tu na ukiwa nacho we unacho tu.

Fikiria Bernard Morrison alicheza kwao Ghana, akacheza Afrika Kusini na DR Congo lakini umaarufu mkubwa ameupata alipokuja kucheza hapa kiasi ambacho hadi kufikia hatua akaongea hadharani kuwa anatamani kuchezea timu yetu ya taifa – Taifa Stars.

Anavutika kuichezea Taifa Stars kwa sababu anaona Tanzania imempa thamani na heshima kubwa kuliko anayoipata katika taifa lake alilozaliwa la Ghana.

Nasikia jamaa amejenga nyumba hapa na ana mpango wa kuishi Tanzania kwa muda mrefu hivyo tayari ameshakuwa mwenzetu na alichobakiza ni kubadili tu uraia rasmi.

Kusajiliwa kwake KenGold ni ishara kuwa bado yupo sana Tanzania hata kama timu kubwa hazina nafasi ya yeye kuzichezea kwa sasa.

Related Posts