Dabo amvuta Bangala AS Vita

SIKU kadhaa tangu amalizane na Azam FC iliyoamua kusitisha mkataba aliokuwa nao, kiungo anayemudu kucheza pia kama beki wa kati, Yannick Bangala amejiunga na AS Vita ya DR Congo inayonolewa na kocha Youssouf Dabo aliyewahi kufanya naye kazi kikosi cha Matajiri wa Chamazi.

Bangala aliyewahi kukukipiga Yanga kabla ya kujiunga na Azam misimu miwili iliyopita, alimalizana na klabu hiyo ya Chamazi mara dirisha dogo lilipofunguliwa ili kumpisha mshambuliaji aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Alassane Diao ikielezwa alilipwa kiasi cha Sh 100 milioni kwa kusitishiwa mkataba huo.

Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa kiungo huyo Mkongo ni kwamba tayari amemalizana na AS Vita baada ya kocha Dabo kupendekeza asajiliwa mara aliposikia kaachwa na Azam walipokuwa wakifanya kazi pamoja miezi kadhaa iliyopita.

Hii si mara ya kwanza kwa Bangala kuichezea Vita kwani alishaitumikia mwaka 2017 ilipomsajili kutoka DC Motema Pembe kisha kwenda FAR Rabat ya Morocco aliyoichezea kabla ya kusajili na Yanga 2022 na mwaka jana ndipo alipotua Azam iliyyoachana naye hivi karibuni. Bangala pia aliwahi kukipiga Les Stars pia ya DR Congo.

“Ni kweli amemalizana na AS Vita ni pendekezo la kocha Dabo ambaye ameuhakikishia uongozi kuwa ataweza kuisaidia timu hiyo kwenye maeneo mengi kuanzia uzoefu alionao pia tayari ameshaichezea timu hiyo anafahamu mambo mengi,” alisema mtoa taarifa huyo aliye karibu Bangala aliyeongeza;

“Kiraka huyo ana uzoefu wa Ligi ya Congo amependekezwa na Dabo na anamuamini kuwa ni mchezaji ambaye anaweza kumpa machaguo kwenye nafasi mbili tofauti hivyo ujio wake ndani ya kikosi cha AS Vita una matumaini makubwa.”

Mtoa taarifa huyo alisema tayari kiungo huyo DR Congo na muda wowote atatangazwa kuwa mchezaji wa AS Vita timu ambayo ameitumikia kwa misimu miwili tofauti.

Related Posts