KIPA Diarra Djigui aliyekuwa nje ya uwanja kwa wiki kama mbili amerejea akianza kujifua, jambo lililompa furaha kocha wa Yanga, Sead Ramovic huku akijiandaa kukabiliana na TP Mazembe ya DR Congo wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga inayoburuza mkia katika Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi moja iliyopata kwenye sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mazembe, ilikuwa na hofu ya kuwakosa nyota wanne wa kikosi cha kwanza akiwamo kipa huyo namba moja, lakini mambo yamebadilika kabla ya kurudiana na Wakongo.
Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli na Chadrack Boka tayari wamesharejea kutoka majeruhi na hofu ikawa kwa Diarra, lakini mambo yamenyooka kwa Ramovic baada ya kipa huyo kuanza mazoezi juzi, na mwenyewe kueleza anaendelea freshi tofauti na hofu iliyokuwapo ya kukaa nje wiki nne hadi sita.
Diarra na Maxi waliumia kwenye mchezo wa Lubumbashi, na ikaelezwa mapema kwamba wangekaa nje kwa muda, lakini kurejea kwao kumeleta mzuka kwa mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo inayohitaji ushindi mbele ya Mazembe ili kuweka hai matumaini ya kufuzu robo fainali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic alisema kila mmoja kwenye timu amefurahia kurejea sio kwa Diarra peke yake, bali hata Musonda, Maxi na Boka.
Kocha huyo aliyeiongoza Yanga katika mechi nane hadi sasa tangu akabidhiwe kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi, ikiwamo michezo mitatu ya CAF na mitano ya Ligi Kuu Bara, alisema Diarra ndiye aliyekuwa anawapa presha, lakini madaktari wamefanya kazi kubwa na wataendelea kuangalia mazoezi yake.
“Tumefurahi kama kikosi kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi, kwani tunakwenda kucheza mechi muhimu wikiendi hii. Hivyo ushindi wa kwanza ni kuwa na kikosi kamili,” alisema Ramovic.
“Ni wazi kuwa presha kubwa ilikuwa kwa Diarra, ila amerudi mazoezini na naamini atakuwa sehemu ya mchezo wa Jumamosi.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Diarra aliyechukua tuzo misimu mitatu mfululizo ikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho, alisema anamshukuru Mungu hali yake imeimarika tofauti na awali.
“Niko sawa kucheza, afya yangu imeimarika na mashabiki wangu wasihofu, Yanga ina kikosi kipana na bora. Tutafanya vizuri tu,” alisema Diarra aliyekuwa akiuguza misuli ya kigimbi cha mguu wa kulia.
Kipa huyo aliyecheza mechi tisa za Ligi Kuu Bara na kupata ‘clean sheet’ saba hadi alipoumia katika mechi za CAF, amekuwa nguzo kwa Yanga tangu aliposajiliwa misimu mitatu iliyopita akitokea Stade Malien ya Mali, Agosti 2021 akiisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu misimu yote mitatu iliyopita sambamba na mingine mitatu ya Kombe la Shirikisho ambapo msimu uliopita alishinda tuzo ya Kipa Bora wa michuano hiyo.
Yanga ikimalizana na Mazembe itakwenda kucheza na Al Hilal ya Sudan kabla ya kuikaribisha MC Alger ya Algeria ambazo katika mechi zote za awali zilishinda kila moja 2-0 mbele ya Wananchi.