Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, imemruhusu Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu Dk Manguruwe anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kwenda kuhojiwa polisi kwa siku tatu mfululizo.
Mkondya na mwenzake, Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59), wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiweno ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Rweyemamu yupo nje kwa dhamana kwa sababu hana mashtaka ya kutakatisha na pia hatahusika katika mahojiano hayo.
Mkondya atahojiwa na maofisa wa polisi kuanzia Januari 6, 2025 hadi Januari 8, 2025, kuhusiana na kesi inayomkabili.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Januari 2, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, baada ya Serikali kuwasilisha ombi mahakamani la kutaka mshtakiwa huyo kwenda kuhojiwa kuhusiana na kesi yake.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, lakini upande wa mashtaka wanaomba Mkondya aletwe mahakamani hapo Januari 6, 7 na Januari 8 kwa ajili ya kuhojiwa na polisi.
“Mheshimiwa hakimu, tunaomba Mahakama yako itoe hati ya kumleta mahakama mshtakiwa aliyepo gerezani kwa sababu Polisi waliomba kuja kumfanyia mahojiano Januari 6, Januari 7 na Januari 8, 2025, hivyo tunaomba amri ya Mahakama ili tuje tumkabidhi kwa maofisa hao,” amedai Wakili Kasala.
Kasala baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Magutu amekubaliana na upande wa mashtaka na kutoa hati ya kuleta mshtakiwa huyo mahakama kwa siku hizo zilizotajwa na alielekeza mshtakiwa ahojiwe na kurudishwa mahakamani akiwa na afya njema na kurudishwa rumande (gerezani).
Baada ya kueleza hayo Hakimu Maguta aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2025 kwa kutajwa.
Katika kesi ya msingi, kati ya mashtaka hayo 28; mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha fedha katika viwanja.
Inadaiwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata fedha mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya kiasi walichotoa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuijipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka 9 ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa katika kipindi hicho alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.
Inadaiwa kuwa Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo akijua ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 5, 2024.