MSAFARA wa TP Mazembe unatua leo nchini tayari kukutana na Yanga katika mchezo ambao kila timu inataka kuweka hesabu sawa kufufua matumaini ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Wakongomani hao kuna chabo wameipiga na kuwashtua.
Baada ya kutambua ina ratiba ya kukutana na Yanga, mabosi wa Mazembe walituma mashushushu ili kupiga chabo katika mechi mbili za Ligi Kuu, lakini moto walioushuhudia umewashtua kwa kubaini soka linalopigwa sasa na vijana wa Jangwani sio kama lile walilocheza siku ya sare ya 1-1 pale jijini Lubumbashi, Desemba 14, mwaka jana.
Mashushushu hao walibaini kuwa wanakuja Tanzania kukutana na timu tofauti kidogo na ile waliyokutana nayo na kufungana bao 1-1 katika mechi ya Kundi A, Prince Dube akichomoa jiooni bao la wenyeji na hilo limefanya benchi la ufundi la Mazembe kuanza kujipanga upya ili kuepuka dozi nene ilizoshuhudia Dar.
Kocha msaidizi wa Mazembe, Pamphil Mihayo ameliambia Mwanaspoti wanajua wanakuja kukutana na Yanga iliyoimarika baada ya kucheza mechi nne za ligi ya nyumbani na kushinda zote kwa idadi kubwa ya mabao na ikicheza kwa kasi tofauti na waliyokutana nayo kwenye Uwanja wa Mazembe.
Mihayo alisema Yanga imebadilika na kurudisha morali ambapo wanakuja kwa tahadhari wakiendelea kupiga hesabu za namna gani wataondoka na ushindi.
Mazembe haijashinda mechi yoyote ya ugenini msimu huu kwenye mechi zake tatu ilizocheza ikipoteza na sare mbili nyumbani matokeo ambayo yanawapasua vichwa mabosi wa timu hiyo, huku Yanga wakivuna pointi moja ugenini katika mchezo dhidi ya Wakongomani hao na kupoteza mbili za nyumbani.
Mihayo alisema wanahitaji kuwazuia Yanga wasiendelee kufunga mabao kama ambavyo wamefanya kwenye mechi za nyumbani, ambapo watajipanga kwenye ulinzi.
Katika mechi nne za Ligi Kuu Bara tangu kilipovaana na Mazembe, kikosi cha Yanga kimefunga mabao 18 na kuruhusu mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Mashujaa, huku kikizifunga kwa mabao 4-0 Tanzania Prisons na Dodoma Jiji na kuifumua Fountain Gate 5-0, ambapo mashushushu wa Mazembe walishuhudia.
“Tuna taarifa za kutosha. Kuna watu wetu wapo hapo. Ukweli ni kwamba tutakuja kucheza mechi ngumu. Unaona jinsi timu yao ilivyoimarika wanafanya vizuri kuliko ilivyokuwa kabla ya kukutana nao hapa kwetu,” alisema Mihayo.
“Timu yao inafunga mabao mengi na kwa sasa ukiangalia mechi tatu za makundi ilifunga bao moja tu dhidi yetu, lakini tunajua mechi tatu zilizopita imefunga mabao zaidi ya 10 bila kuruhusu wavu wao kuguswa. Tunatakiwa kuwazuia vizuri wasiendelee na utulivu huu kwa kuipanga safu yetu ya ulinzi.”
Mihayo aliongeza kuwa, Mazembe haijacheza mechi yoyote ya ushindani tangu ikutane na Yanga wakati wapinzani wao hao wakicheza mechi nne, lakini wanaamini hiyo itawasaidia wachezaji wao kupata utulivu wa maandalizi.
“Ni kweli hatujacheza mechi yoyote tangu tulipokutana na Yanga. Kuna mechi za kirafiki mbili tulizitumia kuwaimarisha vijana ila wenzetu wamecheza za ligi, nadhani wachezaji wetu watakuwa wamepata mapumziko ya kutosha.”
Yanga na Mazembe zinakutana Kwa Mkapa kwa mara ya tatu baada ya awali kukutana mara mbili na kila timu kushinda mchezo mmoja, Wakongomani wakishinda 1-0 mwaka 2016 kabla ya kufumuliwa 3-1 msimu uliopita katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.