Dar es Salaam. Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema miongoni mwa sababu zilizomfanya amteue Jaji Frederick Werema kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni pamoja na kutoa ushauri wenye masilahi ya Taifa.
Kikwete amesema hayo leo Alhamisi Januari 2, 2025 wakati akitoa salamu za pole katika hafla ya kuaga mwili wa Jaji Werema katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Mwaka ule Jaji Mkuu Samatta alileta ombi la kuteua majaji 10, wakati huo kulikuwa na kilio cha upungufu wa majaji na mahakimu… mimi nikawaongezea 10 wengine wakawa 20, miongoni mwao alikuwepo Jaji Werema.”
“Mwaka 2009 nikamteua kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali kwa sababu mara zote mnapokutana anakushauri namna gani mnaweza kuboresha sekta ya sheria na mara zote alikuwa ana shauri kwa kuzingatia masilahi ya Taifa.. Alikuwa mpenda haki,”amesema na kuongeza Kikwete.
Jaji Werema alifariki dunia Desemba 30, 2024 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi