Benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Heroes’ limesema kuwa lengo kuu la kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 yatakayofanyika Pemba, Zanzibar ni kutwaa ubingwa.
Kocha wa Kilimanjaro Heroes, Ahmad Ally alisema kuwa pamoja na ugumu ambao watakutana nao katika mashindano hayo, watahakikisha wanacheza vyema katika mashindano hayo ili wamalize wakiwa na taji.
“Ushindani utakuwa mkubwa kwa sababu kila nchi imejipanga kulingana na matakwa yake nini ambacho inakihitaji kwenye haya mashindano. Naamini hazitokuwa mechi rahisi. Ni mechi ambazo zitaweza kutuweka sisi kwenye yale malengo ambayo tumejiwekea.
“Matarajio ya Watanzania wote hata sisi hapa tulipo ni kufanya vizuri kwa maana ya kuweza kupata matokeo na kikombe. Tunaomba sapoti ya mashabiki kama wanavyofanya siku zote,” alisema Ally.
Kocha huyo alisema fursa aliyoipata ya kuinoa Kilimanjaro Stars ni ya kipekee na atajitahidi kurudisha imani kwa idara ya ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Naishukuru TFF na mkurugenzi wa Ufundi kwa kuniona kwamba ninaweza kuitumikia hii nafasi. Ni fursa kwangu kama Mtanzania kuweza kuisaidia nchi kwa uwezo niliona pia naipongeza klabu yangu ambayo imenipa nafasi ya kuweza kuonekana hadi hapa nilipofika,” alisema Ally.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 yatashirikisha timu tano za taifa ambazo ni Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, na Burkina Faso.
Kilimanjaro Heroes itaanza mashindano hayo kwa kucheza na Zanzibar Heros, Januari 3.