Kilio cha Januari, vifaa vya shule bei juu

Dar/Mikoani. Januari ni msimu wa pilikapilika za maandalizi ya shule. Wazazi na walezi wanahangaika huku na kule kusaka mahitaji, huku bei za bidhaa zikiwa tayari zimepaa.

Kwa wafanyabiashara ni msimu wa kutengeneza faida kupitia vifaa vya shule kutokana na bei kuongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji.

 Baadhi ya wazazi na walezi, huu ni msimu wa changamoto kutokana na wingi wa mahitaji ya vifaa vya shule; vitabu vya masomo, madaftari, kalamu na rula, sare, viatu, soksi na nguo za michezo, achilia mbali ada na gharama za usafiri kwa wanafunzi.

Kwa wale wa kipato cha chini, msimu huu ni changamoto kubwa kwao, kwani hulazimika kufanya kazi za ziada, kuuza mali au hata kukopa fedha, ili kuhakikisha watoto wao hawakosi masomo shule zitakapofunguliwa.

Kutokana na mahitaji hayo, kumekuwa na msongamano kwenye madukani na hata masokoni kunakouzwa vifaa hivyo.

Hata hivyo, hekaheka hizo zinaonyesha umuhimu wa elimu kwa jamii, licha ya changamoto zinazowakabili, wazazi wanajitahidi kwa kila njia kuhakikisha watoto wao wanapata nafasi ya kujifunza na kufanikiwa.

Zikiwa zimebaki siku kadhaa kabla ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa Januari 6 na nyingine Januari 13, 2025 kilio kutoka kwa wazazi na walezi ni kupanda kwa baadhi ya vifaa.

Wakati wazazi na walezi wakilalamikia ongezeko la bei, wafanyabishara wa vifaa vya shule wanatoa wito kwao kufanya manunuzi mapema, kwani kadri siku zinavyokwenda vitapanda zaidi.

Katika maeneo ya Kariakoo, Manzese na Karume, jijini Dar es Salaam, Mwananchi imeshuhudia pilikapilika za ununuzi wa vifaa vya shule.

Mfanyabishara wa jumla na rejareja wa vifaa vya shule eneo la Kariakoo, Sadat Sadi amesema bei imepanda, ikilinganishwa na ya mwaka jana 2024.

Amesema madaftari yaliyokuwa yakiuzwa Sh600 hadi Sh1,000 sasa ni Sh800 hadi Sh1,200, huku yale makubwa ‘Counter Book Quire 2’ yaliyouzwa kati ya Sh1,500 hadi Sh1,800 sasa ni Sh1,800 hadi Sh2,000 kwa bei ya rejareja.

Amesema Counter Book Quire 3 ni Sh2,500 hadi Sh3,000, huku Quire 4 likiwa Sh3,500 hadi Sh4,000 kwa sasa kwa rejareja.

Mfanyabishara mwingine katika eneo hilo, Ally Juma amesema kalamu za wino zimepanda kutoka Sh4,000 hadi kati ya Sh5,000 hadi Sh5,500 kwa dazani, huku penseli zikipanda kutoka Sh1,500 hadi kati ya Sh2,500 na Sh3,000 kwa dazani.

“Niwashauri wazazi kuanza kununua mahitaji ya watoto mapema, kwani kuna wasiwasi wa bei kuongezeka zaidi kadri uhitaji unavyozidi kuwa mkubwa,” amesema.

Simon Mtasha, mfanyabishara wa sare za shule eneo la Manzese anasema mashati, sketi, kaptula na viatu vya shule vimepanda.

Amesema mashati yaliyouzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh8,000 mwaka jana, sasa ni kati ya Sh6,000 na Sh12,000 kulingana na ubora na ukubwa wake.

“Sketi na kaptula awali zilikuwa kati ya Sh4,000 hadi Sh8,000 sasa ninauza kuanzia Sh5,000 hadi Sh10,000,” amesema.

Hata hivyo, amesema wanunuzi bado ni wachache.

Magdalena Thomas, aliyekuwa akinunua vifaa vya shule eneo la Kariakoo kwa ajili ya wanawe wanne, amesema ameshindwa kukamilisha vifaa vyote kutokana na gharama kuwa kubwa.

“Nimefika madukani nikiwa na laki moja yote imeishia kununua mahitaji kidogo ambayo hayawezi kutosheleza watoto wangu wote,” amesema.

Kwa upande wake, Baraka Chelechele, baba wa mtoto mmoja amesema kuna haja ya wazazi kuweka utaratibu wa kununua mahitaji mapema, ili kuepuka gharama kubwa wakati wa msimu wa masomo kuanza.

Baadhi ya wafanyabiashara, wazazi na walezi jijini Mwanza wamelalamikia bei za vifaa vya shule kupanda.

“Soko la vifaa vya shule hata kwa sisi ambao tunanunua kwa bei ya jumla bei imekuwa juu tofauti na mwaka jana, hata ukisema ufanye biashara faida siyo kubwa kama mwaka 2024, ndiyo maana wengi wameamua kufanya punguzo, ili wapate angalau faida kidogo ili mzigo uishe,” amesema Dulla Sakalani, mfanyabiashara wa vifaa vya shule katika Soko la Makoroboi, jijini Mwanza.

“Mfano bei ya shati la ubora wa kati tulikuwa tunanua Sh5,500 lakini sasa ni Sh8,500, shati lenye ubora mkubwa lilikuwa Sh7,500 lakini sasa ni Sh10,000 hadi Sh12,000,” amesema.

Mkazi wa Bugarika, jijini Mwanza, Magret Nelson amesema kutokana na gharama kuwa juu kuna uwezekano wa baadhi ya wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama za vifaa.

“Bei haijashuka, inapanda. Mfano daftari lililokuwa Sh500 sasa ni Sh700, hii ni changamoto kwa mzazi unayesomesha watoto wengi,” amesema.

Mfanyabiashara wa vifaa vya shule katika Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza, Daniel Boaz amesema bei zimepaa kwa kuwa ni msimu wa kuelekea kufunguliwa shule.

“Madaftari Quire 3 tunauziwa katoni Sh75,000 ambayo yanakuwa 36, sisi tunakuja kuuza Sh2,500 lakini bado wateja wanataka tuwauzie Sh2,000 kitu ambacho sisi tutapata hasara. Mwaka uliopita katoni ilikuwa Sh68,000,” amesema.

Licha ya kuwapo malalamiko hayo, muuza vifaa vya shule katika Soko la Makoroboi, Dominic Paul amewataka wazazi kuchangamkia fursa sasa kabla bei hazijapanda zaidi.

Mfanyabiashara katika soko kuu la Chifu Kingalu, Eliabu Joram, amesema kwa sasa wateja wanasuasua akieleza kwa siku anauza sare tatu hadi tano.

“Naamini wiki ijayo tutapata wateja wengi kwa sasa tunajua wazazi wametoka kununua nguo za sikukuu, hivyo wanatafuta pesa nyingine ya kununua mahitaji ya shule kwa watoto wao,” amesema Joram.

Rehema Mwanjonde, mkazi wa Nonde jijini Mbeya amesema shati ambalo mwaka jana lilikuwa Sh5,000 hadi Sh6,000 sasa ni Sh7,000 hadi Sh10,000 kulingana na ubora, huku gauni la shule likiuzwa Sh8,000 badala ya Sh5,000 za awali.

Amesema viatu vyeusi vya shule vinauza kati ya Sh15,000 hadi Sh25,000 kulingana na ubora wake.

Haika Solomon, anayeshona sare za shule amesema bei zinapanda kutokana na gharama za vitambaa na ubora wake.

“Kwa sasa maisha yamepanda, ni tofauti na miaka mingine, kwani kila bidhaa zimepanda kwetu. mafundi na mahitaji ni mengi kama uzi, mafuta ya cherehani na muda mwingi kuandaa nguo,” amesema.

Mkazi wa Mji Mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, Maulid Juma amesema baadhi ya wafanyabishara wanatumia msimu wa kufungua shule kupata kipato zaidi.

Amesema kiatu cha shule walichokuwa wakinunua Sh10,000 sasa kinauzwa kati ya Sh15,000 na Sh20,000.

Mkazi wa mjini Babati, Nurdin Salmin amesema: “Mabegi ya shule unaambiwa kuanzia Sh30,000 na kuendelea bado sare za shule kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na madaftari juu.”

Salumu Massoud, mfanyabiashara jijini Dodoma amesema si bidhaa zote zimezopanda bei.

“Kwenye biashara bei ya vitu vyote kama masweta, mashati na viatu haijabadilika, isipokuwa bei ya kaptura imepanda kidogo kutokana na kupanda kwa bei ya vitambaa,” amesema.

Amesema kupanda bei ya vitambaa kumesababisha kaptura kupanda kutoka kati ya Sh5,000 hadi Sh6,000 na sasa ni Sh8,000.

Damas Makacha, mkazi wa jijini Dodoma amesema kwa sasa bado bei hazijapanda, hivyo wazazi na walezi watumie muda huo bidhaa kabla mambo hayajabadilika.

Imeandikwa na Mariam Mbwana, Anania Kajuni, Hamida Shariff, Hawa Mathias, Joseph Lyimo na Elidaima Mangele

Related Posts