Kwa nini Watanzania huchelewa kufanya manunuzi?

Katika msimu huu wa sikukuu na mapumziko unapoelekea mwisho, kwa siku chache zilizobakia, wengi watajikuta tena wakiwa katika harakati za kwenda masokoni kununua mahitaji ya shule kwa muhula mpya unaoanza. Hali hiyo pia inajitokeza katika misimu ya sikukuu kama Iddi na Krismasi, ambapo kila tarehe ya sherehe inavyokaribia, ni kawaida kuona msongamano mkubwa wa watu katika masoko, maduka na mitaani wakifanya manunuzi ya mahitaji mbalimbali.

Ukiangalia kundi hili la watu, utajiuliza, walikuwa wapi wote hawa? Kwa nini wanasubiri hadi siku za mwisho kufanya manunuzi, licha ya kujua kuwa kutakuwa na msongamano, shida za usafiri na bei za bidhaa kuwa juu?

Moja ya sababu inayochangia jambo hili inaweza kuwa inatokana na saikolojia ya wanunuzi na ninahusianisha na dhana maarufu katika uchumi inayoitwa “temporal discounting”. Kwa mujibu wa dhana hii, watu hupendelea kutimiza mahitaji ya sasa kuliko kupanga kwa ajili ya baadaye. Kwa mfano, wakati wa kupanga manunuzi, wengi huzingatia zaidi mahitaji yanayoonekana kuwa ya haraka kwanza, na manunuzi mengine hufanyika tu wakati itakapokuwa dharura au lazima kununua.

Watanzania wengi, kwa uzoefu wangu, ingawa wanajua kuwa kuchelewa kufanya manunuzi, hasa katika misimu ya sikukuu, kutawaweka katika shida kwa sababu bei zitakuwa zimepanda na kutakuwa na msongamano mkubwa, na mengine, lakini licha ya hayo, watasubiri itakapofika muda wa “lala salama”, kesho au keshokutwa ndio sikukuu au tukio kubwa la sherehe, ndiyo leo watajaa masokoni kufanya manunuzi.

Sababu nyingine ni changamoto za kipato. Watanzania wengi wana vipato vya kawaida na hawana vyanzo vya fedha vinavyotabirika au vya kudumu. Kulingana na taarifa za utafiti wa Finscope mwaka 2023, karibu asilimia 89 ya Watanzania wanajipatia riziki zao kupitia shughuli za msimu, vibarua, au biashara ndogondogo wanazojiajiri wenyewe.

Katika hali hii, inakuwa vigumu kwa familia kupanga manunuzi mapema. Kwa mfano, ni vigumu kujiandaa na mahitaji ya sikukuu inayokuja mwezi ujao, wakati wanahitaji fedha hizo kwa mahitaji muhimu kama chakula. Hivyo, wengi hutegemea kukamilisha manunuzi yao mwishoni, wanapokuwa na fedha, na zaidi tarehe za sherehe ikiwa inakaribia. Tofauti na watu wanaopata mishahara ya kila mwezi, ambao wana uwezo wa kupanga matumizi na kufanya manunuzi yao mapema.

Mfumo wa biashara hapa nchini pia unachangia tatizo hili. Masokoni, kwa mfano Kariakoo jijini Dar es Salaam, wauzaji wengi wa maduka ya nguo, mapambo, viatu na mahitaji mengine ya sikukuu hutegemea kwanza kuuza bidhaa zilizopo madukani ili wakusanye fedha kwa ajili ya kuagiza mzigo mpya, kutoka Dubai, China nk. Hivyo, hata wateja wanaojaribu kununua mapema, kama vile mwanzoni mwa msimu wa sikukuu, wanaweza kukosa bidhaa mpya, fasheni, na mitindo mipya wanayohitaji kwa ajili ya sikukuu. Kauli kama “subiri mzigo mpya, mzigo wa sikukuu unaingia karibuni,” zimekuwa za kawaida.

Matokeo yake, wakati bidhaa mpya zinapofika madukani, mara nyingi huwa ni wiki chache tu kufikia kilele cha sikukuu kama Iddi au Krismasi. Kipindi hicho msongamano madukani, kwenye vibanda vya nguo, na maeneo mengine, unakuwa mkubwa, watu wengi wanaenda kwa pamoja “kusagurasagura”, kila mmoja anawahi kupata kizuri. Ndio utaona madukani na kwenye masoko wauzaji kuongeza muda wa kazi, mfano “tupo mpaka usiku” kuwapa nafasi wateja wanaokuja mwishoni kufanya manunuzi.

Nadharia zinazohusiana na tabia za wanunuzi zinasisitiza umuhimu wa kupanga bajeti mapema na kuepuka ununuzi wa dakika za mwishoni pamoja na ununuzi holela (impulsive buying).

Ununuzi wa “lala salama,” kufanya mnunuzi kwa bei kubwa, uharaka wa kufanya manunuzi inamnyima mteja nafasi ya kufanya maamuzi bora kwa kile anachonunua, na hofu ya bidhaa kuisha inamfanya mtu kununua chochote anachokiona. Mwishowe inaathiri bajeti ya mtu binafsi na familia, ndio utakuta baada ya msimu wa sherehe familia nyingi zinakuwa taabani kifedha, utasikia “nimebaki mweupee”.

Wadau kama taasisi za kifedha na elimu waendeleze juhudi za kutoa elimu ya fedha binafsi, jinsi ya kupanga bajeti na umuhimu wa kupanga manunuzi mapema. Na kuepuka presha kubwa ya manunuzi msimu wa sikukuu, ambalo kibiashara inaonekana ni faida, lakini si lazima itokee kwa namna hiyo.

Related Posts