Mbappe wa Azam apelekwa KMC

UONGOZI wa KMC uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya winga wa Azam FC, Cheickna Diakite ‘Mbappe’ kwa mkopo wa miezi sita, baada ya nyota huyo kuomba kutolewa kwenda timu nyingine ili akapate nafasi zaidi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Taarifa kutoka ndani ya Azam zililiambia Mwanaspoti, Diakite aliyejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Real Bamako ya kwao Mali, viongozi wanataka kumtoa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

“Viongozi wanafikiria kumtoa kwa mkopo kwa sababu bado ni mdogo na hata ukiangalia nafasi yake kikosi cha kwanza imekuwa finyu, wanafikiria kumpeleka KMC kutokana na uhusiano wao mzuri na kocha mkuu, Kally Ongala,” kilisema chanzo hicho.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema hawezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo ingawa kama viongozi walishaanza taratibu zote za kusajili baadhi ya wachezaji, kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha tunaboresha maeneo machache tu kwa sababu hatutaacha wachezaji wengi, pia hata watakaoingia ni vijana ambao tunaamini wana kiu na uchu wa kufikia mafanikio, tukikamilisha tutaweka wazi,” alisema.

Nyota huyo anakumbukwa zaidi msimu wa 2022-23, alipokuja nchini na AS Real Bamako katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo timu hiyo ilipangwa kundi ‘D’ na Yanga na kuonyesha kiwango bora kilichowavutia Azam FC.

Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Fiston Mayele na Jesus Moloko, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 8, 2023.

Msimu huo Yanga iliongoza Kundi D katika michuano hiyo baada ya kukusanya jumla ya pointi 13 sambamba na US Monastir ya Tunisia ila zilitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa huku AS Real Bamako ikishika nafasi ya tatu kwa pointi tano.

TP Mazembe ya DR Congo iliburuza mkia na pointi tatu, huku Yanga ikifika fainali japo ilikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya kupoteza Kwa Mkapa mabao 2-1, kisha kushinda ugenini bao 1-0.

Related Posts