Rais wa Marekani Joe Biden amesema mhusika wa shambulizi la mjini New Orleans alichochewa na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS.
Akinukuu taarifa za Shirika la Upelelezi la Marekani FBI, Biden amesema saa chache kabla ya shambulio mhusika huyo alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii, zinazoashiria kwamba alihamasishwa na IS, akielezea shauku ya kuua.
Soma:Watu 10 wamekufa Marekani baada ya dereva kuparamia umati
FBI imemtambua mshambuliaji huyo kuwa ni Shamsud-Din Jabbar, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 42 kutoka Texas. Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema Jabbar aliwahi kuhudumu katika jeshi kama mtaalamu wa rasilimali watu na mtaalamu wa Tehama kutoka mwaka 2007 hadi 2015 na kisha kikosi cha akiba hadi mwaka 2020.
Alitumwa Afghanistan kuanzia Februari 2009 hadi Januari 2010, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, akiongeza kuwa alikuwa na cheo cha Staff Sajenti mwishoni mwa utumishi wake.
Mkuu wa Polisi Anne Kirkpatrick amemtaja Jabbar kama “gaidi,” huku FBI ikisema “bendera ya IS ilikutwa ndani ya gari lililohusika kuvamia umati wa watu waliokuwa wanasherehekea Mwaka Mpya.
Ripoti inayohusiana: Watu wawili wauawa, wengine kadhaa wajeruhiwa katika shambulizi la bunduki Baltimore
Maafisa wa usalama bado wanatafuta wahusika wengine wa shambuliz hilo lakini hawakutoa maelezo ya kina huku afisa mwanadmizi wa FBI Alethea Duncan akionya kwamba mamlaka “haiamini kuwa Jabbar alifanya uhalifu huo mwenyewe.
Aidha, Rais Biden ameongeza kuwa vyombo vya usalama nchini humo, vinachunguza ikiwa kuna uhusiano wowote kati ya shambulio hilo na mlipuko uliotokea jana nje ya hoteli ambayo sehemu inamilikiwa na Rais mteule Donald Trump huko Las Vegas na kuua mtu mmoja. Trump mara moja alilihusisha tukio la mlipuko nje ya hoteli yake na uhamiaji haramu.
Shambulio hilo limetokea saa chache kabla ya jiji hilo kuandaa mchezo mkubwa wa soka wa Sugar Bowl wa chuo kikuu uliosogezwa mbele hadi leo Alhamis. Mshambuliaji huyo ameuawa katika majibizano ya risasi na polisi baada ya kuwavamia watu.
Soma kuhusu ripoti hii: Watu watano wafariki Ujerumani kutokana na ajali zinazohusishwa na fashifashi
Viongozi mbalimbali ulimwenguni wamelaani shambulizi hilo. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameandika katika ukurasa wa X akisema “hii ni taarifa ya kuhuzunisha kutoka New Orleans”. Ameongeza kuwa “watu waliokuwa wakisherehekea kwa furaha wamevurugwa maisha yao au kujeruhiwa na chuki zisizo na maana.”