Polisi yawafungia leseni madereva 30 kwa ulevi Dar

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewafungia leseni madereva 30 kati ya 179 waliokamatwa katika kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025.

Madereva hao 30 walikamatwa katika operesheni maalumu na walipopimwa walikutwa na ulevi kwa kiwago cha zaidi ya miligramu 80.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Murilo leo Alhamisi, Januari 2, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya usalama jijini Dar es Salaam.

Kamanda Murilo amesema madereva hao walikamatwa na jeshi hilo kabla na baada ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya 2025.

Murilo amesema kipindi cha sikukuu hizo makosa hatarishi ya usalama barabarani ambayo yangesababisha ajali yalidhibitiwa na kuchukuliwa hatua ambapo jumla ya madereva 179 walituhumiwa na kupimwa ulevi.

“Kati ya madereva hao 30 walikuwa na ulevi kiwango cha zaidi ya miligramu 80 kati yao madereva 22 walitokea wilaya ya Kinondoni, sita Ilala na wawili Temeke,” amesema Murilo.

Amesema madereva wenye kiwango kikubwa cha ulevi jeshi hilo limewafungia leseni za udereva kwa kipindi cha miezi sita kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani.

Wakati huohuo, Murilo amesema Desemba 17, 2024 Jeshi la Polisi kanda hiyo linamshikilia Ally Ismail (22), Mkazi wa Kipunguni Mashariki kwa tuhuma za uvunjaji pamoja na wizi wa vitu mbalimbali ikiwemo runinga tatu, ving’amuzi vinne na mashine moja ya kunyunyiza dawa shambani.

Pia amesema katika kipindi cha Novemba hadi Desemba 2024 watu sita wamehukumiwa katika Mahakama mbalimbali za jiji hilo ambapo kati ya hao wawili wamehukumuwa kifungo cha maisha na wanne miaka 30 jela.

Kamanda huyo amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuimarisha mifumo ya ulizia shirikishi ili kuzuia vitendo vya kihalifu.

Related Posts