Ujumbe huo, ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Assaad al-Shibani, Waziri wa Ulinzi Murhaf Abu Qasra, na Mkuu wa Huduma za Kijeshi za Ujasusi Anas Khattab, ulipokelewa Riyadh na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Waleed bin Abdulkarim El-Khereiji.
Shibani alieleza matumaini ya kufufua mahusiano na Saudi Arabia, akisema, “Kupitia ziara hii ya kwanza katika historia ya Syria Huru, tunatarajia kufungua ukurasa mpya, wenye mwanga katika mahusiano ya Syria na Saudi Arabia.”
Mwezi uliopita, maafisa wa Saudi walikutana na kiongozi mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, ambaye anaongoza kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham, ambalo liliendesha mashambulizi yaliyomuondoa Assad tarehe 8 Desemba.
Sharaa, katika mahojiano ya hivi karibuni, alisisitiza nafasi ya Saudi Arabia katika kujenga upya Syria, akisema kuna “fursa kubwa ya uwekezaji kwa nchi zote jirani.”
Soma pia: Syria yamteua kamanda wa HTS kuwa waziri wa ulinzi
Uchumi wa Syria umeharibiwa vibaya na zaidi ya miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, na serikali mpya inakabiliana na changamoto kubwa, kuanzia ujenzi wa miundombinu hadi kushughulikia urithi wa biashara haramu ya dawa za kulevya chini ya utawala wa Assad.
Wanaharakati Douma waandamana kudai haki kwa waliopotezwa
Wakati madaraja ya kidiplomasia yanajengwa nje ya nchi, maandamano yalizuka Douma, mji ulioshuhudia madhila makubwa wakati wa vita, huku wanaharakati wakidai majibu kuhusu hatima ya wanaharakati wanne wa haki za binadamu waliotekwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Waandamanaji walibeba picha za wanaharakati waliopotea—Razan Zeitouneh, Wael Hamada, Nazem al-Hammadi, na Samira Khalil—waliotekwa kutoka ofisini mwao Desemba 2013 wakati wa mwanzo wa vita.
Mwanaharakati Yassin Al-Haj Saleh, mume wa Khalil, alihimiza serikali mpya kuchunguza kutoweka kwao. “Tuna ushahidi wa kutosha kuwahusisha Jaish al-Islam, na tuna majina ya watuhumiwa ambao tungependa wawekwe chini ya uchunguzi,” alisema Saleh.
Wengi Douma wanailaumu Jaish al-Islam, kundi la waasi wa Kiislamu, kwa utekaji huo, ingawa kundi hilo limekanusha kuhusika.
Soma pia: Watawala wapya wa Syria waanza kuwasaka masalia wa Assad
Kwa familia za waliopotea, swali la haki bado linatawala. “Tunatafuta haki, kujua hatima yao, na kuwawajibisha wahusika kwa matendo yao,” alisema Alaa al-Merhi, mpwa wa Khalil.
Zeitouneh, wakili wa haki za binadamu na mshindi wa tuzo ya Bunge la Ulaya mwaka 2011, alikuwa amepokea vitisho kutoka kwa vikosi vya serikali na waasi kabla ya kupotea.
Maandamano haya yanaonyesha majeraha ya kudumu ya vita vya Syria. Douma, iliyokuwa ngome ya waasi, ilikumbwa na uharibifu mkubwa wakati wa vita, ikiwa ni pamoja na kuzingirwa na vikosi vya Assad.
Sasa, wakati Syria inapitia kipindi cha mpito, hatima ya waliopotea inabaki kuwa suala muhimu kwa maridhiano na haki.
Athari za kikanda na kimataifa
Mwaliko wa Saudi Arabia kwa uongozi mpya wa Syria unaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za kikanda. Baada ya miaka mingi ya kuvunja uhusiano na kuunga mkono vikosi vya upinzani, Riyadh ilirejesha mahusiano na serikali ya Assad mwaka jana, na kusaidia Syria kurejea katika Jumuiya ya Kiarabu.
Soma piaKiongozi mpya Syria aahidi kuheshimu mamlaka ya Lebanon:
Hata hivyo, masuala ambayo hayajatatuliwa kama biashara ya captagon—biashara haramu yenye faida kubwa chini ya utawala wa Assad—yanazua changamoto. Serikali mpya inapojitahidi kurejesha uhalali na kujenga upya taifa, itahitaji kusawazisha mahitaji ya ndani ya haki na matarajio ya nje ya utulivu.
Douma na kwingineko, Wasyria wanasubiri majibu—siyo tu kuhusu wapendwa wao waliopotea, bali pia kuhusu mustakabali wa nchi yao iliyoathirika na vita.