“Hizi ni habari mbaya kutoka New Orleans,” ameandika Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwenye ukurasa wake wa mtandao wakijamii wa X, na kuongeza kuwa watu waliokuwa wakisherehekea kwa furaha wameuawa au kujeruhiwa kutokana na na chuki zisizo na maana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio hilo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia na wapendwa wa wale waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema New Orleans imekumbwa na kitendo cha ugaidi huku akitoa pole kwa familia za wahanga na waliojeruhiwa, pamoja na watu wote wa Marekani ambao amesema wanashirikiana kwenye huzuni hii.
Awali New Orleans ilianzishwa na wakoloni kutoka Ufaransa na shambulio hilo lilifanyika katika mtaa maarufu wa Wafaransa katika mji wa Louisiana. Christian Estrosi, meya wa mji wa kusini mwa Ufaransa wa Nice, ambao ulikumbwa pia na shambulio kama hilo mnamo mwaka 2016 na kuua watu 86, ametuma pia salamu za rambirambi.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alitaja pia kusikitishwa mno na shambulio la makusudi dhidi ya wale waliokuwa wakisherehekea Mwaka Mpya huko New Orleans na kusisitiza kuwa hakuna kisingizio cha ghasia kama hizo.
Rambirambi kutoka Uingereza, Ukraine, China,…
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ameandika pia kwenye mtandao wa X kuwa shambulio baya na kushangaza huko New Orleans ni la kutisha huku akitoa pole kwa familia za wahanga, wahudumu wa idara za dharura na Wamarekani wote katika wakati huu wa kusikitisha.
Kwa upande wake, msemaji wizara ya mambo ya nje wa China Mao Ning amewaambia waandishi wa habari kuwa wameshtushwa na shambulio hilo la kikatili na kwamba Beijing daima inapinga vitendo vyovyote vya kikatili na kigaidi vinavyowalenga raia.
Soma pia: Mshambuliaji wa New Orleans alichochewa na IS
Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema ana imani waliohusika na kitendo hiki kiovu watafikishwa mahakamani na kwamba vurugu, ugaidi na vitisho vyovyote kwa maisha ya binadamu havina nafasi katika ulimwengu huu na havipaswi kuvumiliwa. Taarifa za kulaani tukio hilo zimetolewa na mataifa mengine kama Uturuki, Israel na Saudi Arabia.
Rais wa Marekani Joe Biden akinukuu taarifa za shirika la Upelelezi la FBI amesema mhusika wa shambulizi la mjini New Orleans alichochewa na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS na kwamba saa chache kabla ya shambulio, mhusika ambaye ni mwanajeshi mstaafu aliyefahamika kwa jina la Shamsud-Din Jabbar, 42, alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii akielezea shauku ya kuua. Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu 15 na kuwajeruhi makumi ya wengine.
(Vyanzo: AFP, Reuters)