Wadaiwa kuharibu gari la polisi mkesha wa mwaka mpya

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuharibu gari la polisi lililokuwa likifanya doria usiku wa kuamkia Januari Mosi, 2025.

Akizungumza leo Januari 2, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Desemba 31, 2024 Mtaa wa Kiusa, Manispaa ya Moshi, mkoani hapa.

Amesema jeshi hilo linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na baada ya kumaliza watafikishwa kwenye vyombo vya Sheria.

“Tumewakamata watu wanne wako ndani kwa kosa la kuharibu mali kwa sababu walirusha mawe na kuharibu gari letu lililokuwa doria kwa madhumuni ya kuimarisha ulinzi na usalama katika mkesha wa mwaka mpya 2025,” amesema Kamanda Maigwa.

Aidha, Kamanda Maigwa amesema katika mkesha wa mwaka mpya hakukuwa na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani kwa sababu walijipanga kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo hasa yaliyokuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu.

“Tunamshukuru Mungu mkesha wa mwaka mpya ulienda vizuri na hii ni kwa sababu tulijipanga vizuri kwa kuweka doria maeneo mengi.

“Wapo waliokuwa wakitembea kwa miguu kuangalia usalama na waliokuwa wakitumia usafiri wa pikipiki na magari,” amesema Kamanda Maigwa.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, amesema baada ya kundi la vijana kuibuka na kufanya vurugu na kuzuia magari yaliyokuwa yanapita kwa kulala katikati ya barabara kwenye mtaa huo, polisi walifika katika eneo hilo na kutuliza vurugu hizo ambapo vijana hao walianza kupiga mawe gari la polisi na kuharibu vioo vya gari.

“Sisi tulikuwa tumejifungia ndani ghafla tukasikia kelele huku mabomu ya machozi yakipigwa na askari waliofika eneo la tukio kuwatawanya vijana waliokuwa wakifanya vurugu na kurusha mawe,” amesema shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Akizungumzia tukio hilo, diwani wa kata ya Kiusa, Bashiri Tassama amesema lilitokea wakati vijana hao wakisherekea sikukuu ya mwaka mpya.

“Kulitokea vurugu wakati vijana wakisherekea sikukuu ya mwaka mpya na inadaiwa katika vurugu hizo gari la polisi lilipigwa mawe,” amesema diwani huyo

Wakati huohuo, Kamanda Maigwa amesema wanamshikilia dereva wa basi la Ngasere lililogongana na gari dogo aina ya Toyota Noah Wilaya ya Rombo Desemba 26, 2024 na kusababisha vifo wa watu 10 akiwemo dereva wa Noah.

Kamanda Maigwa amesema dereva huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuendesha gari kwa mwendo kasi pia amefungiwa leseni na atafikishwa mahakamani muda wowote.

“Kosa lilikuwa ni la yule dereva wa Noah, lakini dereva wa basi naye alikuwa na makosa kwa sababu alikuwa na spidi kali, sehemu ya kutembea spidi 50 alitembea spidi 85.

“Wamegongana lakini ile Noah isingeweza kuburuzwa na kufinyangwa kiasi kile kama angekuwa kwenye mwendo sahihi.”

Related Posts