*Rais Dkt. Samia asema Jaji Werema alikuwa kiongozi mwenye weledi na msimamo.
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa leo Januari 02, 2025 amemwakilisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika kuaga mwili wa marehemu Jaji Fredrick Werema
ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha
kuanzia Mwaka 2009-2014.
Mheshimiwa
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. Samia amesikitishwa na kifo cha Jaji
Werema na amemtaja kama kiongozi shupavu aliyekuwa anazingatia maadili
wakati wote na mwenye misimamo katika utendaji kazi wake. Tukio la kuaga
Mwili wa Jaji Werema limefanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar
es Salaam.
“Mheshimiwa
Rais anajua kwamba Marehemu amefanya kazi katika mihimili yote na
anauzoefu mkubwa wa utendaji katika mihimili yote, mengi mazuri
ameyatenda, Rais Dkt. Samia anawasihi wote muwe wavumilivu katika
kipindi hiki kigumu na ametusihi tuendelee kumuombea na kuyaenzi yote
aliyoyafanya katika utumishi wake”.
Kadhalika
Mheshimiwa Majaliwa amewataka amewataka wanasheria na watanzania kwa
ujumla kuyaenzi na kuyaendeleza yale yote mazuri aliyoyafanya jaji
Werema enzi za uhai wake”
Kwa
Upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Jaji Werema alikuwa Mwanasheria mbobezi, mzalendo wa dhati
na mara zote alitoa ushauri makini kwa maslahi ya Taifa, alikuwa mahiri
ma mpenda haki. “Amefanya mengi mema kwa Taifa na ameacha alama ya
kudumu nchini, Nilimteua kuwa Jaji kutokana na sifa zake katika
utendaji”
Naye,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema kuwa Marehemu Jaji
Werema alikuwa ni mtu mwenye maono na mtaalam wa Sheria aliyejitolea na
kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sheria na haki zinatumika katika
kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Jaji
Werema alifanya maboresho makubwa katika mfumo wa sheria na haki na
alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha na kuimarisha utawala wa sheria
na kuwaendeleza, kuwafunda na kuwanyanyua wanasheria waliokuwa
wanachipukia, alionesha uongozi wa aina yake katika nyakati ngumu pia
aliweza kupigania maslahi ya Taifa”
Waziri
Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema kuwa Marehemu Jaji Werema
atakumbukwa kwa mengi katika utumishi wake wa umma “Jaji Werema alikuwa
mtu mwenye msimamo, akiamini kitu anafanya na kutenda vile vile, hakuwa
na lugha za kuchanganya, alikuwa muadilifu na alilitumikia Taifa kwa
uwezo wake wote”.
Wakili
Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi amesema kuwa Jaji Werema alikuwa
mahiri na nguzo imara katika sekta ya sheria nchini kwani aliendelea
kuhudumu katika sekta ya sheria hata baada ya kumaliza muda wake
serikali. “Uimara wake katika maeneo mbalimbali ya sheria, uchapakazi
wake umeacha alama katika sekta ya sheria nchini”.