Chanzo harufu mbaya puani | Mwananchi

Dar es Salaam. Umewahi kukutana na mtu, kila akipumua anatoa harufu kali usiyoweza kuivumilia? Wengi huhisi ni jasho la mwili na wachache wakidhani ni harufu ya kinywa. Hii ni harufu itokayo puani.

Huenda ikawa si ugonjwa, ila ni matatizo ya mfumo wa upumuaji yanayofahamika kama halitosis au bad breath, tatizo hili husababishwa na mambo ya kawaida kama uchafu wa kinywa au vyakula vyenye harufu kali na vyanzo vingine vingi.

Baadhi ya tafiti, ikiwemo ile ya ‘American Journal of Rhinology & Allergy’, ilionesha kuwa bakteria na virusi vinavyosababisha maambukizi ya pua (kama vile mafua) vinaweza kuzalisha kamasi na uchafu, ambao hutoa harufu mbaya.

Pia, utafiti wa bakteria kwenye koo na pua, kutoka Journal of Periodontology zimeonyesha namna bakteria wanaoishi kwenye koo, fizi na pua wanaweza kutoa vichocheo vya harufu mbaya puani.

Utafiti mwingine wa Journal of Clinical Investigation (2012) wameeleza namna upungufu wa maji mwilini unavyopunguza uzalishaji wa mate, ambao huathiri mfumo wa upumuaji na kushindwa kupigana na bakteria ili kudumisha usafi wa puani.

Utafiti mwingine kuhusu tabia ya kula kutoka International Journal of Food Sciences and Nutrition uligundua kuwa vyakula vya harufu kali kama vitunguu na vitunguu saumu, ambavyo huliwa mara kwa mara, vinaweza kuathiri harufu inayotoka puani.

Vyakula hivi husababisha kemikali zinazozalishwa mwilini ambazo husafiri kupitia hewa ya pua na kutoa harufu mbaya.

Uchunguzi huo ulibaini pia matumizi holela ya dawa aina ya antibiotiki, husababisha harufu mbaya puani kwa kuathiri kiwango cha bakteria walinzi katika kinywa na kuchochea ongezeko la bakteria hatarishi.

Dawa nyingine ni zile zinazotumika kutibu shinikizo la damu, maumivu au magonjwa mengine nayo huchangia.

Aidha mtaalamu wa masikio, pua na koo Dk Adam Kamonga anasema magonjwa ya pua, koo na kinywa ambayo hutoa harufu mbaya mara nyingi husababishwa na vimbe kwenye mfumo wa pua, koo na hasa saratani.

“Sababu nyingine ni kiungulia, magonjwa ya meno na tatizo la ute mzito kwenye pua ni sababu ya harufu mbaya puani,” anaeleza.

Kamonga anasema tatizo hili huhitimishwa kwa namna mbalimbali ikiwemo usafi kwenye sehemu za koo, pua na meno.

“Mwenye hali hii anapaswa kubadili mfumo wake wa chakula, hasa vinavyomsababishia kiungulia,” anasema pia kudhibiti na kukwepa visababishi vya magonjwa mbalimbali, ikiwemo vyakula vinavyosababisha mzio.

“Ili usifikie kuwa na harufu ya pua ni vyema ukapata ushauri wa kitabibu haraka endapo utaona dalili yoyote ya vimbe mdomoni, pua au kwenye koo,” anaeleza.

Kadhalika anasema tatizo hilo huwapata watu wa rika zote kwa kutegemeana na chanzo, huku waathirika wakitajwa kuwa ni watu wazima.

“Inategemea na aina ya chanzo, ila tatizo hili huwapata zaidi wanaume, kutokana na mazingira yao ya kazi ambapo mara nyingi hukutana na visababishi vya harufu hiyo,” anaeleza Dk Kamonga.

Mtaalamu wa afya, Dk Isaya Muhando anasema unaposikia harufu inatoka mdomoni au puani mtu huyo ana bakteria walioathiri njia ya hewa.

“Bakteria wanaposhambulia, sehemu ya ndani ya mfumo wa pua, mara nyingi ndiyo harufu huanza kutoka, ikiambatana na maumivu makali ya kichwa,” anasema Muhando.

Anasema, mfumo huo, unapoathiriwa zaidi huleta madhara kwenye mfumo wa sikio na ubongo na hata kupata madhara aina ya meningitis.

“Meningitis ni maambukizi yanayoshambulia sehemu zinazofunika ubongo, na hii hutokana na bakteria kushambulia mfumo mzima wa upumuaji na kisha kuathiri na mifumo mingine, ikiwemo ubongo,” anasema.

Aidha, Muhando anasema mtu anapokumbwa na tatizo hilo anashauriwa kumuona mtaalamu wa sikio, pua na koo.

“Tatizo hili huchukua muda kutibiwa, na pengine mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu zilizoathiriwa na bakteria hao,” anaeleza.

Anasema mtu mwenye harufu mbaya puani anahatari kubwa ya kuathiri mfumo wa ubongo kutokana na ukaribu uliopo baina ya mfumo wa pua na ubongo.

Sambamba na hilo, Muhando anasema, watu waliopo hatarini kupata tatizo hilo ni wale wenye mzio wa mfumo wa upumuaji na wale wasiotibu tatizo la mafua.

Related Posts