MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Majimaji, Yanga, Polisi Tanzania na Taifa Stars, Ditram Nchimbi amejiunga na Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu huu.
Nchimbi amejiunga na Mbeya Kwanza baada ya kuikacha Biashara United kutokana na timu hiyo kukabiliwa na ukata.
Mbeya Kwanza katika Championship msimu huu imevuna pointi 24 katika mechi 14 ikikamata nafasi ya sita, ikishinda michezo saba, sare tatu na kupoteza nne, huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 13.
Nchimbi aliachana na Biashara akiwa ameifungia mabao mawili katika ligi hiyo.
Biashara kwa sasa inaburuza mkia ikiwa na alama moja katika mechi 14 baada ya kupokwa pointi 15 kufuatia kutotokea kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nchimbi alisema anautumia muda huo wa miezi sita kurejesha kiwango na utimamu wa mwili, ili kupata soko kwenye dirisha kubwa la usajili, huku akiwaahidi mashabiki wake kuwa sasa amerudi rasmi.