Ishara hizi katika kucha hutabiri hali ya afya yako

Dar es Salaam. Licha ya kucha kuwa urembo asili unaoongeza uzuri kwenye miguu na vidole vya mikono kwa binadamu na wanyama, wataalamu wa afya wanataja kuwa zina taarifa muhimu kuhusu hali ya afya ya binadamu.

Ni muhimu kuzingatia mabadiliko ya rangi kwenye kucha zako, na vipengele vingine vinavyotumika kama tahadhari kwa magonjwa mengi.

Mabadiliko kwenye muonekano wa kucha, kama vile rangi, umbo au muundo wake, yanaweza kuwa ishara ya mwanzo kabisa ya matatizo ya kiafya yanayotokea mwilini au ishara ya afya bora uliyonayo.

Pia, kucha nene na ngumu mara nyingi ni ishara ya afya nzuri na lishe bora, wakati kucha dhaifu na rahisi kuvunjika yanaweza kutabiri upungufu wa vitamini au madini muhimu mwilini mwako.

Huku, kucha ngumu na kali hutafsiriwa kama ishara ya afya njema ya mwili na mzunguko mzuri wa damu.

Hata hivyo, tafiti mbalimbali kutoka sehemu kadha wa kadha zimethibitisha namna kucha zinavyokuwa na utabiri sahihi wa kile kinachoendelea mwilini, ikiwa huna sababu nyingine ya nje ya mwili inayosababisha kucha hizo kubadilika na kutoka kwenye asili yake.

Hata hivyo, kucha zilizoegemea upande, inaweza kuonyesha matatizo ya mzunguko wa damu mwilini.

Pia, wataalamu wa afya hutumia kucha kama sehemu muhimu ya kuelewa afya ya mtu, hii ni kutokana na sehemu hiyo, kuwa na utabiri wa magonjwa mengi yanayohusiana na mifumo ya mwili, kama vile mfumo wa mzunguko wa damu, ini, mapafu na mfumo wa kinga mwilini.

Moja ya tafiti kuhusu kucha ni ile ya British Medical Journey ya mwaka 2007 iliyoonyesha kuwa mabadiliko ya umbo la kucha kuwa mviringo, ni moja ya viashiria vinavyohusishwa na magonjwa ya moyo na mapafu.

Magonjwa mengine ni ugonjwa wa mapafu, pumu ya mapafu, mapafu kujaa maji na magonjwa ya moyo kama matatizo ya muundo wa moyo.

Aidha, kucha kuwa mviringo kama kijiko, baadhi ya tafiti ikiwemo ile ya National Institute of Health (NIH) ya mwaka 2005 ilithibitisha kuwa ni moja ya upungufu wa madini chuma ambapo husababisha tatizo la anaemia.

Kadhalika, utafiti uliofanywa na Journal of the American Academy of Dermatology ya mwaka 2002, ulithibitisha kuwa mstari unaojitokeza kando ya kucha ni dalili ya majeraha makubwa au maambukizi ndani ya mwili.

Mstaari huo unaofahamika kama Beau’s lines kwa mujibu wa tafiti, hutokea zaidi kwa wagonjwa wa saratani, wagonjwa wa moyo au wakati wa maambukizi ya magonjwa ya homa ya matumbo na wenye upungufu wa virutubisho vya zinki.

Aidha, utafiti mwingine wa mwaka 2006 kutoka Journal of Nephrology, ulibainisha kuwa hali ya kucha kuwa na mzunguko mweupe karibu na msingi wa kucha ambao kitaalamu huitwa Terry’s nails, mara nyingi huwatokea watu wenye matatizo ya figo na ini.

Mtaalamu wa Mifupa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk William Mgisha anasema mwonekano wa kucha unaweza kutafsiri magonjwa zaidi ya 50 kwenye mwili wa binadamu.

“Ubora na mwonekano wa kucha unaweza kutoa tathmini ya afya ya binadamu, hasa kwenye utendaji kazi wa baadhi ya viungo mwilini,” anaeleza.

Anasema kucha ambazo ubora wake ni hafifu, mara nyingi mhusika yuko kwenye hatari ya kupata magonjwa kadha wa kadha au tayari amepata magonjwa hayo.

Kadhalika anaongeza kuwa kwa mwonekano wa kucha asili, kuna alama ya nusu duara kwenye kiungio cha kucha au shina la kucha, ila ukubwa au udogo wa alama hiyo, pia ni ishara ya baadhi ya magonjwa.

“Alama nyeupe ikikuwa na kufikia nusu ukucha basi tayari mtu huyo ni mgonjwa wa figo au yuko mbioni kupata ugonjwa huo,” anasema Dk Mgisha.

Kubadilika kwa umbo la kucha, na kuwa na shepu ya rungu au kijiko ambayo kitaalamu huitwa (finger clubbing) nayo ni dalili ya upungufu wa damu wa muda mrefu.

“Aina hii ya kucha, pia huwa ni dalili ya matatizo ya mapafu au magonjwa ya muda mrefu ya mapafu,” anaeleza.

Anasema, kucha hueleza afya ya mtu na hitilafu mbalimbali zinazotokea ndani ya mwilini na si nje ya mwili.

Mgisha anasema kucha zinapaswa kuwa imara kwa wakati wote na zisiwe nyepesi au kuvunjika kwa haraka.

“Mtu anapokuwa na kucha nyepesi, mara nyingi ni moja ya dalili za ukosefu wa maji ya kutosha mwilini, ambapo husababisha matatizo ya figo, japo kucha huvunjika ila uvunjikaji wake uwe na chanzo, bila hivyo kucha zinapaswa kuwa ngumu ili zitafsiriwe kuwa na afya njema,” anaeleza.

Sambamba na hilo Mgisha anasema watu wasipuuzie mabadiliko yoyote yanayotokea kwenye kucha.

“Magonjwa ya mapafu, figo au moyo na magonjwa mengine ya muda mrefu haya, hayaji bila dalili zozote, magonjwa haya ni mchakato wa muda mrefu, ambao dalili zake huonekana kupitia kucha,” anaeleza.

Anasema, kabla ya magonjwa hayo kuleta athari kubwa, wengi wanakuwa na dalili zote za mwanzo zinazoashiria tatizo la baadhi ya viungo vya mwili.

Kadhalika anaongeza kuwa, waathirika wakubwa wa hali hii ni wale wenye magonjwa ya muda mrefu kama figo, pumu, sukari, seli mundu na saratani ya damu na kuwa, wengi wenye saratani ya mapafu kucha hujikunja mfano wa kijiko.

Utafiti wa mabadiliko haya, kama vile kucha zinazovunjika, kuwa na madoa, au kubadilika rangi, unaweza kusaidia kugundua magonjwa mapema na hivyo kujipatia huduma ya mapema na matibabu bora zaidi.

Kadhalika, American Liver Foundation ya mwaka 2003 pia, ilithibitisha kuwa kucha zenye rangi ya njano, ambapo kitaalamu huitwa Jaundice, mara nyingi zinahusishwa na matatizo ya ini kama vile uvimbe kwenye ini au ugonjwa wa ini utokanao na pombe.

Jaundice hutokea wakati ini linaposhindwa kusafisha sumu na kuitoa mwilini na hivyo kusababisha kiwango cha sumu kuongezeka na kisha kuathiri rangi ya kucha na ngozi.

Pia, kucha za bluu au kijivu, zinatajwa kuwa ni kati ya ishara ya upungufu wa oksijeni katika damu.

Hali hii inaweza kumtokea mtu mwenye matatizo ya mapafu, pumu au matatizo ya mfumo wa damu au shinikizo la damu na moyo.

Pia, makucha yenye rangi ya zambarau au nyekundu, mara nyingi huwa ishara ya shida.

Tafiti zinaonyesha upungufu wa virutubisho, kama vile chuma, zinki, na vitamini B12, ni moja ya sababu zinazoweza kuathiri ukuaji wa kucha.

Tafiti nyingi zimethibitisha ukosefu wa virutubisho unavyoathiri muundo na ukuaji wa kucha na kwamba hali hiyo ni dalili ya anemia, ambapo mwili hukosa oksijeni ya kutosha kutokana na ukosefu wa seli nyekundu za damu mwilini.

Kirutubisho kingine kinachoathiri ukuaji wa kucha ni ukosefu wa vitamini B12 na ukuaji wa kucha pia, unaweza kuwa na uhusiano na afya ya jumla ya mwili wa binadamu.

Ikiwa kucha zinakua kwa upole au zinaonekana dhaifu, inaweza kuwa ishara ya upungufu wa virutubisho kama vile protini, chuma au vitamini B12.

Pia, inaweza kutokea, kutokana na magonjwa ya kibinadamu kama vile ugonjwa wa ngozi au matatizo ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Mabadiliko katika hali ya kucha yanaweza pia kutofautiana kulingana na umri, watoto wanaweza kuwa na mabadiliko madogo katika ukuaji wa kucha kutokana na mabadiliko ya kimwili au chakula.

Watu wazima, kwa upande mwingine, wanapaswa kuwa na uangalizi zaidi juu ya mabadiliko katika kucha, kwani yanaweza kuonyesha hali mbaya ya afya kama vile saratani au magonjwa sugu ya moyo.

Related Posts