Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC) tawi la Tanzania imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari ili kufanikisha utekelezwaji wa shughuli mbalimbali inazozifanya nchini kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu tathmini ya utendaji wa shughuli za kampuni hiyo, Kiongozi wa CCCC Tawi la Tanzania, Li Yuliang, amesema wamepata mafanikio makubwa kupitia shughuli wanazozifanya na kuvipongeza vyombo vya habari kwa kuhabarisha umma matukio ya kampuni hiyo.
Majadiliano hayo yamehusisha waandishi na wahariri wa vyombo vya habari kutathmini shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo pamoja na kujadili changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo.
“Ni matumaini yangu kuwa mwaka 2025 tutaimarisha ushirikiano, kujenga uhusiano bora na kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi,” amesema Yuliang.
Katika mkutano huo kampuni hiyo ilieleza malengo yake, mafanikio na michango ya kijamii kwa mwaka 2024.
Kampuni hiyo inatekeleza miradi mbalimbali Masasi – Mtwara, Arusha na Dar es Salaam ambako inatekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Mbali ya shughuli za ujenzi pia imekuwa ikihamasisha jamii kujifunza lugha ya Kichina ikitembelea shule na vyuo kisha kuzungumza na wanafunzi pamoja na kugawa vitabu.
Kampuni hiyo pia imekuwa ikitembelea makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu, watoto yatima na kuwapa misaada ya kibinadamu.