KOCHA mpya wa Singida Black Stars, Hamdi Miloud amekiri kibarua alichonacho baada ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo sio rahisi, licha ya kufurahia kukutana na wachezaji wenye ubora na uwezo mkubwa ambao anaendelea kuwasoma kabla ya kuanza mambo katika Ligi Kuu baadae Machi, mwaka huu.
Licha ya kuwa na uzoefu na mafanikio katika soka la Afrika, Miloud atakutana na mitihani katika majukumu mapya ya kuiongoza Singida inayolenga kumaliza msimu miongoni mwa timu nne bora katika Ligi Kuu Bara ili kushiriki michuano ya kimataifa. Hii ni baadhi ya mitihani atakayokutana nayo.
Ligi Kuu Bara ni michuano yenye ushindani mkubwa. Singida Black Stars inashika nafasi ya nne kwa pointi 33 nyuma Simba (40), Yanga (39), na Azam (36). Ligi imesimama, lakini baada ya mapumziko duru la pili litakuwa na ushindani zaidi.
Miloud atakutana na vigogo Simba, Yanga na Azam ambao wamekuwa na rekodi nzuri na kujivunia wachezaji wenye ubora wa kimataifa. Lengo la Singida Black Stars ni kumaliza miongoni mwa timu nne bora za ligi, lakini hili halitakuwa jambo jepesi.
Nini cha kufanya? Miloud anatakiwa kujenga kikosi thabiti ili kushinda michezo muhimu dhidi ya timu kubwa.Mwenzake Patrick Aussems, alifutwa kazi baada ya timu hiyo kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga na kutoka sare dhidi ya Coastal.
Miloud ana miezi miwili ya kuandaa timu na kumaliza msimu kwa mafanikio.
Kocha huyo atahitajika kuhimiza wachezaji kufanya kazi kwa bidii na kuwa na umoja ili kuhakikisha wa-na-shinda michezo muhimu. Pia, atahitaji mabadiliko katika mfumo wa kiufundi na mbinu.
Singida Black Stars inahitaji kuwa na kikosi chenye nguvu kila idara. Miloud atahitajika kutoa nafasi kwa wachezaji na kuhakikisha wanapata mazoezi ya kutosha ili kuwa na ushindani katika kila mchezo.
Kocha huyo atakutana na changamoto ya kusimamia usajili wa wachezaji wapya na kuhakikisha wanaendana na mfumo wake wa ufundi. Singida Black Stars itahitaji kufanya usajili wenye tija kwa kuongeza wachezaji wenye ubora kimataifa na kuendeleza vipaji vya ndani.
Ikiwa Singida Black Stars itakutana na changamoto ya kuwa na wachezaji wachache wa kiwango cha juu Miloud atalazimika kuwatumia vizuri waliopo kuendeleza uwezo kwa kiwango cha juu.
Miloud atahitajika kuhakikisha kuwa uongozi, wachezaji na mashabiki wanakuwa kitu kimoja. Hii ni muhimu kuhakikisha timu inapata matokeo bora.
Uhusiano mzuri kati ya kocha, wachezaji na mashabiki utaleta hamasa kwa timu.
Miloud ana rekodi nzuri katika michuano ya kimataifa ambako amefika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 akiwa na USM Alger, huku robo ikiwa mara mbili akiwa Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya lile la Shirikisho Afrika.
Mbali na USM Alger pia alizinoa JS Kabylie ya Algeria, Al- Salmiya ya Kuwait, TP Mazembe ya DR Congo, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al- Ettifaq FC ya Saudia Arabia.
Kocha huyo mwenye Leseni ya UEFA A aliyerithi mikoba ya Patrick Aussems alisema amekamilisha tathmini ya awali ya kikosi na kugundua asilimia kubwa ya wachezaji wana uwezo kuendana na falsafa zake.
Miloud mwenye jukumu la kuhakikisha timu hiyo inamaliza nafasi nne za juu, aliwataka wachezaji kuwa tayari kwa mabadiliko, huku akiwahakikishia kwamba anaamini wanaweza kufikia malengo ikiwa watacheza kwa umoja na kujituma kwa bidii.
Akizungumza na Mwanaspoti, Miloud alieleza kwamba analenga kutambulisha mfumo wa soka la kuvutia na linaloshambulia kwa nguvu.
“Tuna timu yenye vipaji vikubwa na nimejionea uwezo. Soka ni zaidi ya kushinda michezo tu, ni kutoa burudani kwa mashabiki,” alisema kocha huyo.
“Lengo langu ni kuhakikisha timu inacheza soka la kuvutia ambalo litawafanya mashabiki wa Singida Black Stars kujivunia timu yao. Ili kufikia hili lazima tufanye kazi kwa bidii na kila mchezaji atahitajika kuonyesha kiwango cha juu cha ufanisi.”
Katika majukumu aliyopewa, Miloud alisisitiza hakuna njia ya mkato katika kufanikisha malengo hayo. “Nitahakikisha tunajiandaa vyema kwa kila mechi na kufuata mipango yetu kwa umakini. Timu itacheza soka la kushambulia, lakini pia tutakuwa na umakini mkubwa katika ulinzi,” aliongeza kocha huyo.
Mastaa wa Singida Black Stars wanatarajiwa kurejea kambini baada ya wiki mbili ili kuendelea kujiandaa na mikiki ya Ligi Kuu Bara. Singida Black Stars inadaiwa imemsajili straika Jonathan Sowah kutoka Al-Nasr ya Libya, ili kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Elvis Rupia.
Timu hiyo inashika nafasi ya nne kwa pointi 33 kweny msimamo wa Ligi Kuu Bara.