Kigi Makasi achimba mkwara Championship

KIGI Makasi, nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Mtibwa Sugar aliyetua Stand United ‘Chama la Wana’ amesema wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo wamekula kiapo cha kushinda mechi za nyumbani, huku akiichimba mkwara Geita Gold watakayoivaa katika mchezo wa kufungia duru la kwanza la Ligi ya Championship.

Makasi alijiunga na Chama la Wana dirisha dogo lililofunguliwa Desemba 15, 2024 sambamba na Lucas Sendama, Khalid Kibailo, Aniceth Revocatus, Seleman Richard, Omary Issa, Ramadhan Said na Ashraf Malolo.

Stand inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa Championship ikiwa na pointi 29 kupitia michezo 14, ikishinda tisa, sare mbili na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 18 na kufungwa 11.

“Malengo yetu kwa mechi za nyumbani ni kupata ushindi kila mchezo japo ni kazi ngumu, lakini wachezaji, viongozi na mashabiki hapa Shinyanga tumejipanga kutimiliza lengo hilo,” alisema Makasi.

“Mechi ijayo ni muhimu zaidi tunakwenda ugenini kucheza na timu iliyo juu yetu, tunahitaji nguvu ya mashabi na tutajipanga vizuri tushinde, tunawaomba tu mashabiki wajitokeze kwa wingi. Nimecheza muda mrefu tunaelewa hali ilivyo, hivyo inatusaidia kuwakumbusha wengine nini cha kufanya tukiwa uwanjani.”

Naye Sendama alisema wanapata matokeo mazuri kwa sasa inatokana na wachezaji wote kufuata vyema maelekezo ya benchi la ufundi, na jambo zuri zaidi ni kwamba timu nzima ina ushirikiano mkubwa, hivyo, wapo tayari kwa mapambano ugenini na nyumbani.

Kaimu Kocha Mkuu wa Stand United, Feisal Hau alisema; “Hii timu ni nzuri na inaendelea kupambana. Bado tuko sehemu salama na tunataka kuhakikisha tunamaliza duru la kwanza tukiwa sehemu salama zaidi. Tunashukuru uongozi unatusaidia kufanikisha haya.”

Related Posts