Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ametaja umahiri wa sheria na misimamo katika kutaka haki kuwa miongoni mwa mambo yaliyomshawishi kumteua Frederick Werema kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2006.
Kikwete amesema hayo leo Januari 2, 2025 kwenye hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jaji mstaafu, shughuli iliyofanyika viwanja vya Karimjee Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa.
Jaji Werema aliyeshika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 2009 hadi 2014, alifariki dunia Desemba 30, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Kikwete amesema Jaji Werema aliteuliwa katika wadhifa huo na wenzake 20 pamoja na mahakimu kujibu kilio cha wakati huo cha uhaba wa wataalamu hao.
“Sifa zinazotajwa kwa Jaji Werema ndizo zilizonishawishi mwaka 2006 nimteue kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
“Mwaka ule Jaji Mkuu Barnabas Samatta alileta kwangu maombi ya kutaka majaji 10 lakini wakati ule kulikuwa na kilio kikubwa cha upungufu wa majaji na mahakimu.”
Amesema kilio cha upungufu wa wataalamu hao kilijengwa na hoja ya kwamba kuna ucheleweshaji hukumu za kesi zilizokuwa mahakamani.
“Nilipozungumza na Jaji Mkuu Samatta, jawabu lake lilikuwa ni kuongezewa majaji na mahakimu wa ngazi nyingine na wakati ananiletea mapendekezo hayo mwaka wa fedha ulikuwa umepita nusu yake, lakini uzuri wake kulikuwa na mishahara ya miezi sita ambayo haijatumika,” amesema.
Amesema aliridhia ombi hilo na kumuahidi kuwaongezea majaji wengine 10 ili kufikia idadi ya 20, kwa kuwa mishahara yao ilikuwepo.
“2006 ulikuwa mwaka wa kwanza kwa Mahakama kupata majaji 20 na mmoja wao alikuwa Jaji Werema na wakati wote ilikuwa ukikutana naye alikuwa na mawazo ya namna gani ya kuboresha tasnia ya sheria na kusimamia Serikali,” amesema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema mwaka 1998, Jaji Werema aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa masuala ya Katiba na haki za binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria ambako alionyesha umahiri.
Amesema katika nafasi hiyo aliratibu marekebisho ya Katiba na kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na alishiriki kikamilifu katika mageuzi ya michakato ya uchaguzi.
“Jaji Werema amechangia kuimarisha mifumo ya sheria na utawala bora pamoja na kuandaa mikataba mbalimbali ya kimataifa kwa niaba ya Serikali,” amesema.
Hamza ametaja miongoni mwa baadhi ya kazi alizowahi kufanya Jaji Werema ni sheria ya mabadiliko ya Katiba, sheria ya tume ya mabadiliko ya Katiba, sheria ya uchaguzi.
“Nyingine ni Sheria ya Mtoto, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na Sheria ya Madini,” amesema.
Pia Hamza amebainisha kuwa Jaji Werema ni miongoni mwa wanasheria waliokuwa wanaongoza mazungumzo ya kupata suluhu ya mgogoro wa ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
“Katika timu hiyo na mimi nilikuwepo alikuwa anatupa ushauri mzuri mazungumzo yalikuwa yanafanyika Maputo Msumbiji alikuwa mwenye uzalendo mkubwa,” amesema.
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi amesema katika kesi ya Ziwa Nyasa, Jaji Werema alikuwa mstari wa mbele, huku wakieleza mambo yote aliyoyafanya yataendelea kutumika katika sekta ya sheria.
“Ameacha miongozo mizuri inayoendelea kutumika, kuna maamuzi kama 28 aliyoyatoa yenye tija ambayo tunaendelea kuyatumia kama marejeo,” amesema.
Mwili Werema umesafirishwa leo kuelekea mkoani Mara, ambapo mazishi yatafanyika nyumbani kwake Wilaya ya Butiama Jumamosi Januari 4, 2025.