KOCHA wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema hadi sasa timu hiyo ya jijini Mbeya iko katika mwelekeo mzuri, hasa baada ya kuwanasa aliyekuwa kipa wa Biashara United, Diey Makonga na mshambuliaji Mtanzania, Kelvin George aliyetokea AS du Port ya Djibouti.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema licha ya kikosi hicho kushika nafasi ya pili na pointi 31, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar yenye 35, bado wana kazi ya kufanya, ingawa usajili wa nyota hao na wengine utaongeza matumaini kwao.
“Ushindani umekuwa mkubwa sana na ukiangalia tumefanya maboresho ya eneo la ulinzi na ushambuliaji ili kuongeza balansi ya kikosi chetu, bado tunaendelea na usajili tukiamini huu ni msimu wetu utakaotupa karata ya kurejea Ligi Kuu Bara.”
Mayanga aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Mtibwa Sugar Agosti 5, 2023, alisema kasi ya washindani wao inampa nafasi nzuri ya kukisuka vyema kikosi hicho, akiamini hadi sasa hakuna mwenye uhakika wa kupanda Ligi Kuu moja kwa moja.
“Ukiangalia gepu la pointi lililopo halikupi uhakika wa kujihakikishia utapanda Ligi Kuu na isitoshe mzunguko wa pili ndio ambao ni mgumu zaidi kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu, tutapambana kadri ya uwezo wetu ili kufikia malengo.”
Timu hiyo ya jijini Mbeya imecheza michezo 14 hadi sasa ambapo kati ya hiyo imeshinda 9, sare 4 na kupoteza mmoja tu, ikifunga mabao 27 na kuruhusu 14, ikisaka tiketi ya kurudi tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka 2022-23.