PAZIA la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 ambayo kwa msimu huu imehusisha timu za taifa, linafunguliwa leo usiku kwa mchezo mmoja unaozikutanisha timu ‘ndugu’ za Tanzania Bara na Zanzibar, huku Uganda The Cranes ambao ni moja ya wenyeji wa Chan 2025 na Afcon 2027 ikijiondoa katika dakika za mwishoni.
Michuano hiyo inayofanyika kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, sasa imesaliwa na timu za nchi nne tu, baada ya awali Burundi kuchomoa na kuwafanya wenyeji kushindwa kuiingiza Sudan Kusini kuziba pengo kabla ya jana tena kuwepo kwa taarifa kuwa, Uganda The Cranes imechomoa kuja kushiriki michuano hiyo.
Kutokana na kujitoa kwa Burundi na Uganda, kumelazimisha wenyeji wa michuano hiyo kupangua ratiba na sasa leo itapigwa mechi kati ya Zanzibar Heroes ambao ni wenyeji dhidi ya Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara, kabla ya kesho Burkina Faso na Harambe Stars Kenya kumalizana, mechi zote zikipigwa kuanza saa 2:15 usiku.
Pambano la leo linatabiriwa ugumu kutokana na timu zote mbili kufahamiana kwa kuundwa na wachezaji wanaofahamiana na wanaocheza katika Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda wa miezi miwili kupisha michuano hiyo na ile ya Fainali za CHAN itakayofanyika mwezi ujao katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Juzi na jana vikosi vya timu hizo zinazonolewa na makocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ kwa Zanzibar Heroes na Ahmad Ally wa Kilimanjaro zilikuwa zikipasha mazoezi ya mwisho kabla ya kuvaana leo kuanza kusaka pointi za kuwapeleka fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Januari 13, siku moja baada ya sherehe za Siku ya Mapinduzi Zanzibar inayoadhimisha Miaka 61 tangu yafanyike Januari 12, 1964.
Kili Stars itashuka uwanjani leo ikiwategemea nyota kama Crispin Ngushi, Edgar Williams, Ayoub Lyanga, Metacha Mnata, Lameck Lawi, Nassor Saadun, Zidane Sereri, Lusajo Mwaikenda na Offen Chikola, wakati Zanzibar itakuwa na vichwa hatari kama Maabad Maulid, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Laurian Makame, Ame Ibrahim, Adeyum Saleh, Issa Mukrim na wengine.
Timu hizo zilipokutana mara ya mwisho mwaka jana zilishindwa kutambiana katika ufunguzi wa Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja baada ya kutoa suluhu, lakini mechi ya baina ya timu hizo huwa ni vita kwelikweli kutokana na timu hizo kufahamiana na upinzani uliopo miongoni mwa wachezaji.
Kesho Jumamosi utapigwa mchezo kati ya Burkina Faso na Kenya kabla ya Jumapili kuwa mapumziko kabla ya wenyeji Zanzibar Heroes kurudi uwanjani Januari 6 kuvaana na Burkina Faso, huku Kili Stars itacheza siku inayofuata dhidi ya Kenya na kumaliza ratiba Januari 19 dhidi ya Burkina Faso, ilihali Kenya na Zanzibar zitaumana Januari 10 na Januari 11 na 12 itakuwa ni siku za mapumziko na fainali itapigwa Januari 13 kwa timu mbili zitakazokuwa zimemaliza na pointi nyingi ili kupata bingwa.
Msimu uliopita katika michuano hiyo kwa ngazi ya klabu, Mlandege ilitetea ubingwa kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0, baada ya awali kutwaa taji hilo 2023 kwa kuifunga Singida Big Stars kwa mabao 2-1 katika fainali kali zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.