KLABU ya Namungo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa KenGold, Joshua Ibrahim baada ya kufikia makubaliano binafsi na nyota huyo, aliyekitumikia kikosi hicho cha jijini Mbeya kwa mkataba wa miezi sita tu.
Straika huyo ndiye kinara wa mabao wa wageni hao wa Ligi Kuu wanaoburuza mkia kwa sasa akiwa na mabao manne. Alijiunga na KenGold kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Tusker ya Kenya, ingawa kulikuwa na kipengele kilichokuwa kinamruhusu kuondoka katika dirisha hili dogo akipata timu nyingine mpya.
“Nilisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuniruhusu kuondoka nikipata timu nyingine ingawa Namungo nimekuja kwa mkopo na sio mkataba wa moja kwa moja, ni wakati mwingine mzuri kwangu wa kutafuta changamoto mpya,” alisema Joshua.
Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema bado hawajakamilisha usajili wa mchezaji mwingine zaidi ya waliowatangaza na kama watafanikisha wengine wataweka wazi, japo taratibu za kuboresha kikosi hicho katika dirisha hili bado zinaendelea.
“Wachezaji wote tuliwaosajili tumeshawatangaza katika mitandao yetu ya kijamii hivyo, kama Joshua ni miongoni mwa nyota tuliowapata dirisha hili tutawaweka wazi, tunaboresha kikosi chetu kutokana na mapendekezo ya benchi letu la ufundi.”
Mbali na Joshua, nyota wengine wapya waliojiunga na timu hiyo ya ‘Wauaji wa Kusini’ ni Issa Abushehe ‘Messi’ aliyekuwa anaichezea KVZ FC ya visiwani Zanzibar, Derrick Mukombozi na Emmanuel Charles waliorejea tena ndani ya kikosi hicho.
Wengine ni beki wa kati Daniel Amoah aliyewahi kutamba na Azam FC, kiungo, Najim Mussa aliyetokea Singida Black Stars na winga wa Simba, Salehe Karabaka aliyejiunga kwa mkopo kwa ajili ya kuongeza nguvu timu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda.