Mpanzu sasa uhakika, Mutale akiachwa Dar

KIKOSI cha Simba tayari kipo jijini Tunis, Tunisia kikijichimbia katika hoteli moja ya kishua iitwayo Royal Asbu, huku benchi la ufundi pamoja na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakipa mzuka zidi baada ya Shirikisho la Soka Afrika kuwalainisha mambo kabla ya kuvaana na CS Sfaxien Jumapili ya wiki hii.

Simba iliyoondoka juzi usiku kwenda Tunisia ikipitia Uturuki, inaendelea kujifua kwa mazoezi ya mwisho mwisho ikiwa na mziki kamili wa wachezaji 22 chini ya Kocha Fadlu Davids.

Ikiwa inahesabu saa kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, uliopo jijini Tunis, Tunisia, mapema mchana wa leo kambi hiyo ilipata furaha baada ya kuletewa taarifa juu ya kupitishwa kwa jina la winga Mkongoman, Ellie Mpanzu kuanza kuitumikia timu hiyo katika mechi za kimataifa za CAF.

Taarifa zilizotolewa na Simba ni kwamba, Mpanzu aliyetumika katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, ameruhusiwa kuitumikia timu hiyo katika mechi za CAF, ambapo Jumapili hii kikosi hicho kitavaana na Sfaxien katika mchezo wa Kundi A.

Mpanzu ambaye hajafunga bao lolote wala kuasisti katika Ligi ametumika kwa dakika 189, ni mmoja ya nyota 22 waliosafiri na timu hiyo hadi Tunisia kwa ajili ya pambano hilo, jambo lililowapa mzuka mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wakiamini wing huyo Mkongoman atawasaidia katika mechi hiyo ya ugenini.

Kupitia jumbe zao mbalimbali za mitandao ya kijamii mara baada ya Simba kuachia taafifa za Mpanzu kupata ruksa ya kuitumikia timu hiyo kimataifa, mashabiki na wanachama wameonyesha furaha wakiamini kuna kitu ataongeza katika kikosi hicho kilichoshinda mechi mbili za nyumbani na kupoteza moja ya ugenini.

Simba ilianza kwa kuinyoa Bravos do Maquis ya Angola kwa bao 1-0 kisha kulala 2-0 dhidi ya CS Constantine ya Algeria na kuifunga Sfaxien katika mechi ya kwanza Kwa Mkapa kwa mabao 2-1 na Jumapili zitarudiana kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, uliopo jijini Tunis, Tunisia.

Mapema jana, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kikosi kilifika salama na kuanza kujifua kikiwa na wachezaji 22 walioambatana na timu hiyo akiwamo Mpanzu, lakini kiu kubwa waliyonayo ni kutaka kushinda ugenini kwa mara ya kwanza msimu katika michuano ya CAF, kwani mechi moja ya raundi ya pili ililazimishwa suluhu la Al Ahli Tripoli ya Libya na ile ya makundi ilipoteza mjini Constantine, Algeria.

Inaelezwa kuwa CAF imepitisha jinma la Mpanzu aliyeanza kuitumikia Simba kupitia dirisha dogo la usajili, lakini aliyekosa mchezo wa kwanza wa Simba na Sfaxien uliopigwa Desemba 15 siku ilipofunguliwa dirisha hilo na pia aliikosa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KenGold kabla ya kuanza kutumia ilipovaana na Kagera SUgar ugenini na kushinda mabao 5-2, huku akitumika kwa dakika 57.

Mambo yakiwa freshi kwa Mpanzu, kwa upande wa Mutale ameendelea kukumbwa na majanga baada ya kuumia tena nyama za paja na kumfanya akae nje kwa muda wa wiki kama nne, hali inayomfanya kukosa mechi zote za kimataifa Simba ukiwamo mchezo wa Jumapili hii dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Mutale ni mmoja ya wachezaji walibakishwa jijini Dar es Salaam wakati kikosi kikisafiri hadi Tunisia kuwahi pambano la Kundi A la Kombe la Shirikisho, ikielezwa kuwa anajiuguza kwa kuumia mazoezi ikiwa ni kipindi kifupi tangu arejee kutoka kwenye majeruhi yaliyokuwa yamemuweka nje ya uwanja.

Mzambia huyo alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Power Dynamos ya Zambia lakini tangu atue amekuwa hana mwendelezo wa kucheza mara kwa mara kutokana na majeraha ya mara kwa mara inaelezwa alipata shida hiyo akiwa mazoezini na kushindwa kucheza dhidi ya Singida Black Stars.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa winga huyo sio sehemu ya kikosi kilichosafiri hii ni kutokana na kuhitaji mapumziko na uangalizi mzuri kutokana na jeraha alilonalo.

“Nafikiri atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nne au zaidi ili kuweza kurudi kwenye hali yake ya utimamu ni nzuri kwake kwasababu ligi imesimama lakini hawezi kuwa sehemu ya wachezaji wapambanaji wanaosaka nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali kombe la Shirikisho Afrika,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Kusimama kwa ligi kwa muda wa miezi mitatu kutamfanya ajiuguze kwa usahihi na atarudi akiwa fiti na kuendeleza mapambano kama bado atakuwa ndani ya kikosi hiki kwasababu lolote linaweza kutokea.”

Mutale alisajiliwa kwa mbwembwe katika dirisha kubwa la msimu huu, lakini ameshindwa kufanya maajabu akiwa hana bao lolote katika Ligi Kuu, kitu kinachoelezwa kimewafanya mabosi wa klabu hiyo kufikiria kumpiga chini.

Licha ya kukosekana kwa Mutale ndani ya Simba, benchi la ufundi halina presha kutokana na uwepo kwa Mpanzu anayecheza sambamba na Kibu Denis na Ladack Chasambi, mbali na uwepo wa Edwin Barua.

Related Posts