Katika kuadhimisha mwaka mpya, tunapata nafasi ya kutafakari na kufanya mabadiliko chanya katika maisha yetu. Wengi hutumia kipindi hiki kupanga malengo na mikakati mipya na ni muhimu kukumbuka kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni kudhibiti viwango vya sukari.
Ulaji wa sukari kupita kiasi ni moja ya changamoto kubwa za kiafya zinazoongezeka duniani na kuleta madhara makubwa kama kisukari cha aina ya pili, magonjwa ya moyo na matatizo ya figo.
Katika mwaka huu mpya, ni muhimu kuwa na mikakati bora zaidi ya kudhibiti sukari, ili kuepuka madhara haya na kuishi maisha bora.
Mwaka mpya unakuja na fursa ya kuanzisha mikakati mipya ya kudhibiti afya zetu. Kama ilivyo kwa malengo mengine, mikakati ya kudhibiti sukari inahitaji kuwa na mpango maalum na ushawishi wa kufanya mabadiliko.
Mwaka huu unapaswa kuwa mwanzo wa mabadiliko. Hii inaweza kuwa fursa nzuri ya kujitolea kwa lengo la kula vyakula vyenye virutubisho bora kama vile matunda, mboga za majani, nafaka zisizokubolewa na vyakula vya protini.
Mikakati ya afya ya mwaka huu inapaswa kuzingatia upunguzaji wa vyakula hasa vya viwandani ambavyo vimehusishwa na ongezeko la magonjwa sugu.
Lishe bora inabaki kuwa nguzo kuu katika kudhibiti viwango vya sukari. Kila mwaka, wengi wetu hufanya maazimio ya kuboresha lishe yetu, lakini mara nyingi tunakutana na changamoto za kutekeleza malengo haya kwa ufanisi.
Hivyo, mwaka huu, tunapaswa kuwa na mikakati madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuzingatia ulaji wa vyakula vya kiasili na kupunguza vyakula vyenye sukari nyingi.
Kunywa maji ya kutosha, vinywaji vya asili kama juisi ya matunda ambazo hazina athari kubwa katika viwango vya sukari mwilini. Inashauriwa kula mlo kamili asubuhi, mchana na jioni, ili kusaidia mwili kutumia sukari kwa kiwango cha polepole na hivyo kudhibiti uzalishaji wa insulini.
Mazoezi ni sehemu muhimu ya mkakati wa kudhibiti viwango vya sukari. Kadri tunavyofanya mazoezi ya mara kwa mara, ndivyo tunavyoongeza matumizi ya sukari mwilini kupitia misuli.
Mazoezi husaidia pia kuboresha utendaji kazi wa seli za mwili, ambazo zinahitaji sukari kwa ajili ya nishati. Mazoezi ya wastani ya angalau dakika 30 kwa siku yanaweza kusaidia kuyeyusha sukari mwilini na kuepusha magonjwa mengine yanayohusiana na kisukari.
Kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kuwa na nidhamu katika ulaji vyakula, kunasaidia kudhibiti viwango vya sukari na kuepuka matatizo makubwa ya kiafya yanayohusiana na sukari.