Mwinyi amjibu Othman tuhuma za ufisadi, deni la Taifa

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amejibu tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kuhusu ufisadi na ongezeko la deni la taifa lisiloendana na kazi zinazofanyika.

Rais Mwinyi amejibu madai hayo leo Januari 3, 2025 wakati akifungua kituo cha mabasi cha Kijangwani, akisema licha ya maendeleo yanayofanyika, wapo watu (hakuwataja) wanataka kumkatisha tamaa kwa kusema maneno ya uongo na uzandiki lakini hayatamyumbisha.

Januari mosi, 2025 akizungumza na waandishi wa habari, Unguja alipotangaza nia ya kugombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Othman pamoja na mambo mengine, alisema kuna ufisadi mkubwa ambao unafanyika na kuna madeni ambayo wakopeshaji wa kimataifa na nchi haina uwezo wa kuyalipa.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu (BoT), kati ya mwaka 2020 hadi 2023, deni la Taifa lilipanda mara tatu kwa asilimia 208 kutoka Sh887 bilioni hadi kufika Sh2.397 trilioni.

Kiongozi huyo alifafanua kwamba: “Kwa maneno mengine, kila Mzanzibari sasa ana deni la angalau Sh119, 850, fedha ambazo tunadaiwa na wakopeshaji wa kimataifa na bado hatuwezi kuonyesha fedha hizo zilitumika kwa ajili gani.”

Akizungumza baada ya kufungua kituo hicho, Rais Mwinyi amesema Serikali inakopa kwa nia njema kufanya miradi ya maendeleo na kwamba maneno yanayosemwa na wapinzani ni ya uongo na hayamyumbishi katika kutekeleza majukumu yake.

“Wakati tunafanya haya yote, kuna maneno yanayotoka kwa wapinzani ya kutaka kutukatisha tamaa, nataka leo niwaambie hadharani kwamba mimi siyumbishwi, sijawahi kuyumba wala sitayumba. Maneno mnayoyasema kwanza ni uongo. Nataka niwafahamishe ukweli leo, maana propaganda nyingine zinatiwa uongo zilete taabu,” amesema.

Waache uongo, waache unafiki, waache uzandiki na waache fitina,” amesema Dk Mwinyi akishangiliwa.

Ameongeza kuwa: “Wakati tunaingia madarakani deni lilikuwa Sh800 bilioni, baada ya miaka minne sasa hivi deni limepanda hadi Sh1.2 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 50 na siyo asilimia 208 kama inavyoelezwa.”

“Lakini imesemwa kwamba kila Mzanzibari kwa sasa amebebeshwa deni la Sh119, 000, lengo lao ni kutengeneza sura ionekane sote tunadaiwa, lakini nataka niwaambie kwamba ambacho hawakusema hawa ndugu zetu, tuna akaunti maalumu ya kulipa madeni, mbona hawaizungumzi?

Dk Mwinyi ameongeza kuwa: “Wakati tunazungumza leo hii ndani ya akaunti ile zipo Dola za Marekani 250 milioni, sawa na karibu Sh600 bilioni, sasa kama unazo kwenye akaunti yako Sh600 bilioni na unadaiwa Sh1.2 trilioni, maana yake deni lako linahimilika na unaweza kukopa tena na tena.”

Amesema Serikalio imejiwekea utaratibu maalumu wa kutenga dola 10 milioni kila mwezi kuweka kwenye akaunti hiyo, kwa mwaka ni dola 120 milioni, sawa na karibu Sh300 bilioni. Amesema kama wanadaiwa Sh1.2 trilioni na kwenye akaunti kuna Sh600 bilioni, maana yake uwezo wa kuzipata hizo Sh600 bilioni ni miezi miwili.

Kama hilo halitoshi, amesema kila mwezi wanakusanya Sh300 milioni “sasa tunaogopa nini kukopa ili tufanye miradi ya maendeleo?

Huku akishangiliwa na waliohudhuria hafla hiyo, Dk Mwinyi amesema: “niwaulize, ni nchi gani duniani ambayo haikopi, hao wakubwa Marekani, Uingereza na Ufaransa ndiyo wenye madeni makubwa kuliko sisi hapa, lazima ukope ilmradi uwe na uwezo wa kulipa.”

Kipindi cha miaka minne tangu Serikali iingie madarakani, wamelipa mafao ya Sh250 bilioni na wamewekeza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh300 bilioni huku akisema wameweka fedha zao kwenye benki zaidi ya Sh700 bilioni.

“Ukisikia mfuko unafanya vizuri, unatakiwa uwe na takwimu kama hizo, kwenye mafao wapo kwenye maendeleo wapo, hongereni sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, na kama wasingefanya hivyo, ningewashanga maana mfuko huu kazi yake sio kukusanya pesa na kuziweka, kazi yake ni kuhakikisha wanaboresha mafao na wanakuwa sehemu ya maendeleo ya nchi yao,” amesema.

Rais Mwinyi amesema kwa sasa kuna mpango mpya wa usafiri wa kisasa wa umma katika mji wa Zanzibar baada ya kukaa wakaona umuhimu huo mkubwa, hivyo ikaonekana watafute maeneo ya kujenga vituo vya kisasa ili kutimiza azma ya kuwa na usafiri wa kisasa.

“Ndugu zangu wakati tunaadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi, hatuwezi kuendelea kuwa tunatumia magari ya shamba kuwa mjini, ipo sababu ya magari yale kuitwa ya shamba, yanakuwaje mjini? Lazima magari ya mjini yawe ya mjini,” amesema.

Amesema ukienda nchi yoyote duniani zilizoendelea huwezi kukuta chai maharage zipo katikati ya mji na Zanzibar imeazimia mjini kutakuwa na mabasi ya umeme ya kisasa.

“Ninapokuwa ninasema Zanzibar kutakuwa kuna mabasi ya umeme, treni na teksi za kwenye maji, wanafikiri ninatania, kabla ya mwisho ya mwaka huu tutapanda mabasi ya umeme hapa Unguja na ndio maana tunataka vituo vya kisasa viendane na mabasi tunayozungumzia,” amesema.

Pamoja na Kijangwani, amesema kwa sasa kinajengwa kituo cha mabasi hayo ya kisasa, pia kitajengwa Jumbi, Mwanakwerekwe na Mwera ambayo itakuwa njia kuu mtu akitaka kwenda mikoa yote anatumia usafiri huo.

Amesema ndani ya mji watahitaji vituo vingine vya ziada: “Leo ukienda pale karibu na ofisi ya chama (CCM) utakuta vurugu iliyopo watu wakisubiri usafiri, hatuwezi kuendelea namna hiyo.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kutakuwa na vituo vya kisasa Kijangwani, Malindi, Hospitali ya Mnazimmoja na Michenzani.

Akizungumzia urasimu ambao umetajwa kukwamisha maendeleo, kiongozi huyo amesema urasimu katika Serikali usiokuwa na sababu sasa mwiko.

“Narudia kusema, hii sasa ni mara ya mwisho na mtu yeyote anayetaka kufanya miradi ya maendeleo akikutana na urasimu katika taasisi yoyote aje kwangu moja kwa moja, hatuwezi kukaa mwaka mmoja, miaka miwili tunazungumza jambo moja, hatuna muda huo, tuzungumze wiki moja mambo yafanyike.

Kauli hiyo ilikuwa ikijibu changamoto iliyoelezwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Nassoro Shaaban Ameir wakati akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa kituo hicho, akisema licha ya miradi mikubwa wanayojenga, changamoto kubwa wanayokutana nayo ni urasimu kutoka kwa taasisi za Serikali.

“Mheshimiwa Rais, kwa kweli kuna changamoto moja, hii inaniumiza sana, urasimu kwa baadhi ya taasisi za Serikali, sipo hapa kwa ajili ya kuwasema, maana naona hata wakuu wengine wa taasisi wapo hapa, lakini hili limekuwa tatizo kubwa,” amesema.

Pia, mkurugenzi huyo amesema mwisho wa mwezi, wastaafu 15,000 wanalipwa pensheni zaidi ya Sh5 bilioni.

“Hizi fedha hazirudi, tunawapa. Tunadumisha uchumi na amani na utulivu, kwa hiyo tusipolipa, siku moja kutakuwa na vurugu hapa nchini,” amesema.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema licha ya kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na wanasiasa, kwamba mfuko huo hauna uwezo wa kulipa wastaafu na fedha zao zimetumika kutengenza miradi, amesema wamefanya tathmini na kubaini ZSSF ina uwezo kulipa mafao ya wastaafu kwa miaka 25 ijayo bila kufanya uwekezaji wowote.

Kuhusu mikopo, amesema, “hawajui mikopo inayochukuliwa ndiyo inajenga nchi, hawajui unavyowekeza zaidi, ndio thamani ya nchi yako inavyokua, kutoka mwaka 2020 thamani ya nchi imekua kwa kiasi kikubwa.”

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil amesema uchumi wa Zanzibar unategemea huduma za utalii na usafirishaji.

Amesema katika sekta ya huduma peke yake kwa mwaka 2019, ilikuwa na mchango wa asilimia 51.

“Ndani yake kuna utalii na usafirishaji. Tunategemea itakua zaidi na itachukua sekta zingine za uchumi na kusaida zingine kama kilimo,” amesema.

Related Posts