PIRAMIDI YA AFYA: 2025 wazee wafanye mazoezi mepesi zaidi

Heri ya mwaka mpya 2025 kwa wasomaji wote wa gazeti hili katika kona ya afya.

Leo jicho la kitabibu litawapa ufahamu kuhusu mazoezi mepesi kwa wazee, ambayo wakiyafanya mwaka huu 2025 yatasaidia kuboresha afya ya mwili, hatimaye kuwakinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Umri wa miaka 60-65 kuendelea huchukuliwa kama umri wa uzee, yaani kipindi ambacho wengi wanakuwa tayari wamestaafu kazi.

Umri unaposogea na kufikia uzee, haimaanishi kufanya mazoezi kwa ajili ya afya ya mwili ndiyo basi tena. Wazee, kama walivyo watu wengine wanahitajika kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara ili kuwa na afya njema.

Ni kweli kwa baadhi ya wazee kufanya mazoezi kuna changamoto mbalimbali, ikiwamo udhaifu wa viungo kutokana na kutumika na kulika.

Ikumbukwe kuwa hata mzee anapofanya mazoezi mepesi humsaidia kuwapunguzia hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, ikiwamo kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Uzee unapowadia ni vyema kujua mazoezi mepesi ambayo ni rahisi kuyafanya kuendana na hali ya uzee. Zoezi la kutembea au kukimbia taratibu ni zoezi rahisi lenye matokeo makubwa kwa afya ya mwili.

Wazee wafanye zoezi hili kwa siku tano za wiki kwa dakika 30 kwa siku au kutembea umbali wa kilomita mbili kwa siku.

Kama kutembea barabarani au viwanjani ni kikwazo, wanaweza kutumia mazingira ya nyumbani au ofisini kufanya matendo ambayo yanautembeza au kuushughulisha mwili.

Kwa wenye uwezo wanaweza kutumia mashine ya ndani ya kukimbilia au kutembelea ijulikanayo kama Cardio machine.

Unapoamka asubuhi kaa kwa dakika 3-5 halafu vuta pumzi ndefu na kutulia, kisha taratibu anza kunyoosha viungo vya mwili kwa dakika 5 hadi 10, hii inasaidia kunyoosha viungo na kuuandaa mwili na siku mpya.

Baada ya hapo unaweza kutumia chumba unacholala kutembea umbali mfupi mara nyingi kwa kuzunguka kwenda na kurudi katika eneo hilo.

Badala ya kutumia zaidi rimoti kuwasha TV, AC na feni tembea kwenda kuwasha kila mara unapohitaji kubadili chaneli au kuongeza joto au kuongeza kasi ya feni.

Epuka kutumia lifti, badala yake tumia ngazi za kawaida, pia unaweza kutumia ngazi zilizopo katika nyumba za kuishi angalau kupanda kwa dakika 20 kila siku.

Punguza matumizi yasiyo ya lazima ya vyombo vya usafiri kwenda umbali wa karibu, badala yake tembea, mfano kwenda dukani au nyumba za ibada.

Mkusanyiko wa matendo haya kwa siku huwezesha kufanya mazoezi ya kutembea pasipo kujijua. Ili kufikia malengo inahitajika angalau kutembea hatua 10,000 kwa siku.

Zoezi la pili ni kuogelea, kwa wazee wanaojua kuogelea ambao wako maeneo ya kando kando ya ziwa, bahari au vituo vyenye mabwawa ya kuogelea, wanaweza kufanya zoezi hili.

Zoezi hili linashika namba moja kwa kushughulisha viungo vingi vya mwili kuliko zoezi lolote.

Zoezi la tatu ni kunyanyua vitu vyenye uzito wa wastani na mazoezi ya viungo vya mwili. Zoezi maarufu la viungo ni yoga ambalo asili yake ni India, zoezi hili lina ufanisi mkubwa kuimarisha afya ya mwili. Mazoezi mengine ambayo yanaweza kuwafaa wazee ni pamoja kuendesha baiskeli za ndani, kufanya kazi za usafi wa mazingira na bustani.

Mazoezi haya yakifanywa kwa umakini huwafanya wazee kuimarisha afya ya mwili, hivyo kuchangia kuendelea kuishi maisha marefu zaidi.

Mazoezi haya yanasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yana gharama kubwa kuyatibu.

Related Posts