Kyiv. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema wanajeshi wanakimbia eneo la mapigano dhidi ya vikosi vya Russia hususan kipindi cha mwaka 2024 ambapo taifa hilo limekumbwa na uhaba wa wapiganaji wa akiba.
Ripoti hiyo inadai kubaini uwepo wa wanajeshi wanaokimbia maeneo ya kambi zao za kijeshi kwenye uwanja wa mapambano bila kupewa ruhusa hususan ni kipindi hiki ambacho vikosi vya Russia vinaendelea kusonga mbele eneo la Donbass.
Tovuti ya Russia Today, imeripoti kuwa Novemba pekee, wanajeshi wa Ukraine zaidi ya 100,000 walifunguliwa mashtaka kwa kosa la kukimbia vita maeneo mbalimbali nchini humo.
Hata hivyo, Russian Today ilitahadharisha kuwa huenda namba halisi ikawa inavuka idadi ya wanajeshi 100,000 waliofunguliwa mashtaka hayo.
Akizungumza katika Kituo cha Televisheni cha Telemarathon nchini Ukraine, Zelensky alikiri kuwepo visa vya wanajeshi hao kutoroka mapigano hususan mwaka 2024, hata hivyo amesema idadi ya wanaokacha mapigano hayo imepungua.
“Kesi za wanajeshi wanaoshtakiwa kwa kosa la kukimbia mapigano mwaka 2024 ziliongezeka, lakini tangu Septemba au Oktoba, visa hivyo vilipungua,” alisema Zelenskyy.
“Vita ya muda muda mrefu ni ya muda mrefu tu. Watu wetu wana jitahidi kuvumilia na kupambana, lakini wameanza kuchoka kila mahali,” alisisitiza Zelenskyy.
Katika hatua nyingine, Zelensky alisema kuchoka kwa wanajeshi hao kunachangiwa na uhaba wa wapiganaji, jambo linalosababisha waliopo makambini kupigana kwa muda mrefu bila kupumzishwa hatimaye kutafuta mbinu mbadala ya kupumzika ambayo ni kutoroka.
“Hatuna askari wa akiba wa kutosha. Kwa nini? Kwa sababu siyo kila wanaochukuliwa wanafaa kuwekwa kama wanajeshi wa akiba,” alisema.
Gazeti la Financial Times limelipoti kuwa moja ya sababu kuu ya wanajeshi hao kukimbia mapigano kuwa ni kutopewa mapumziko ama likizo, jambo linalowafanya waone kutoroka kama ndiyo njia pekee ya kupata muda wa kupumzika.
Ili kukomesha vitendo vya wanajeshi kutoroka mapigano huko Ukraine, Serikali ilifanya vitendo hivyo kuwa kosa la jinai kuanzia juzi, Januari Mosi, 2025.
Mapema mwaka huu, Ukraine ilishusha umri wa wanaotakiwa kuajiriwa Jeshini kutoka miaka angalau 30 hadi miaka 25 kwa lengo la kuongeza idadi ya wanajeshi na kujihakikishia kuendeleza mapambano dhidi ya uvamizi wa Russia katika mipaka na miji ya nchi hiyo.
Vipande vya video vimekuwa vikisambaa kwenye mitandao ya kijamii vikionyesha makundi ya wanajeshi wakikimbia vituo vyao vya mapigano huku wengine wakikamatwa. Video nyingine zinawaonyesha maofisa wa Jeshi la Ukraine wakisaka vijana kwa nguvu mitaani kwa ajili ya kuwaingiza jeshini.
Wakati huohuo, Marekani imekuwa ikisisitiza kuishauri Ukraine kushusha umri wa kujiunga jeshini hadi miaka 18 ili kuongeza idadi ya wapiganaji hususan ni wakati huu ambao utawala mpya wa Marekani uko kwenye hatihati ya kutoendelea kuikingia kifua Ukraine kwenye vita hiyo.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Idara ya Upelelezi nchini, Ukraine, Tatyana Sapyan amesema ofisi hiyo imeanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma za wanajeshi wa kikosi cha 155 kinachopewa mafunzo na wapiganaji kutoka Ufaransa.
Sapyan alitoa kauli hiyo jana Alhamisi ambapo alisema kwa mujibu wa Taarifa za ndani ya jeshi, wanafanya uchunguzi wa madai ya kuwepo wanajeshi wanaokimbia mafunzo na mapigano katika uwanja wa vita dhidi ya vikosi vya Russia.
Kauli hiyo ya Sapyan, imekuja siku chache tangu mkufunzi wa kijeshi katika kambi ya mafunzo yanayorayibiwa na Ufaransa, Yury Butusov, kudai kuwa zaidi ya wanajeshi 1,700 wametoroka mafunzo katika kambi hiyo.
Tangu Russia itangaze kuanza Operesheni yake nchini Ukraine imefanikiwa kutwaa mikoa zaidi ya mitano ya Ukraine ikiwemo Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, Pokrovisk na Crimea ambayo ilitwaliwa tangu mwaka 2014.
IMEANDIKWA NA MGONGO KAITIRA KWA MSAADA WA MASHIRIKA.