Mbeya. Uongozi wa shule ya sekondari ya Ivumwe iliyopo jijini Mbeya, umemwangukia Rais Samia Suluhu Hassan ukimwomba asaidie uboreshaji wa miundombinu ya shule hiyo ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia katika elimu.
Shule hiyo inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imekuwa ikipata matokeo mazuri kitaaluma ambapo kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2024 ilishika nafasi ya tano kitaifa na ya kwanza kimkoa.
Hata hivyo, licha ya matokeo hayo, hali ya miundombinu ya shule hiyo imeelezwa kutokuwa rafiki hasa upande wa madarasa na maabara, jambo linalotishia kushuka kwa taaluma na ustawi wa wanafunzi wake.
Jitihada mbalimbali zinafanyika kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa maabara za kisasa, hata hivyo bado inakabiliwa na ukata ili kukamilisha malengo yao ya kutoa elimu bora inayoendana na wakati.
Akizungumza na Mwananchi Januari Mosi, 2025, Mkuu wa Shule hiyo, Oscar Mwaihabi amesema kutokana na changamoto ya uchakavu wa miundombinu hasa ya maabara, tayari bodi imeanzisha ujenzi ili kukabiliana na tatizo hilo.
Amesema licha ya msaada wanaopata kutoka CCM katika usimamizi, lakini nguvu imekuwa ndogo kwani hadi kukamilika kwa vyumba vitatu vya maabara hizo sambamba na ofisi za walimu, inahitajika zaidi ya Sh40 milioni.
“Kwa gharama ya ujenzi wa jumla ni zaidi ya Sh90 milioni, lakini tulipofikia inahitajika zaidi ya Sh40 milioni, tunamuomba Rais Samia na wadau wengine watusaidie kukamilisha hili.
“Malengo yetu ni kufikia Februari 2025 tuwe tumemaliza kwa kuwa wanafunzi wanafungua shule Januari 13, kitaaluma tunafanya vizuri lakini tatizo ni miundombinu yetu,” amesema Mwaihabi.
Kwa upande wake, mwalimu wa masomo ya sanyansi shuleni hapo, Mrisho Mbombwe amesema kukosekana kwa vifaa na miundombinu ya kufundishia inaweza kuathiri kiwango cha taaluma kwani licha ya kusoma, inahitaji kufanyika vitendo.
Amesema maabara iliyopo haikidhi ubora na kiwango stahiki kwa maisha ya sasa katika sayansi na teknolojia huku akieleza kuwa hata vifaa vya kufundishia havitoshi.
“Maabara inayotumika haikidhi, vifaa havitoshi, sayansi inahitaji kusoma na kufanya kwa vitendo, vinginevyo kiwango cha ufaulu kitaaluma lazima kishuke,” amesema Mbombwe.
Naye mwalimu msaidizi wa taaluma katika shule hiyo, Morice Oduka amesema uwapo wa maabara ya kisasa utaongeza kasi ya ufaulu kwa sababu mazingira yatakuwa rafiki, amewaomba wadau kusaidia ukamilikaji wa ujenzi huo.
“Hizi ni maabara za kisasa zinazokidhi mahitaji, tukifundisha katika mazingira mazuri mwanafunzi anapata uelewa zaidi na ufaulu wetu utapanda kwani licha ya nafasi ya tano mwaka huu tunataka ya kwanza mwakani,” amesema Oduka.
Mmoja wa watumishi wakongwe shuleni hapo, Proscus Joseph ‘Mangi’ amesema uongozi wa sasa umeonyesha mabadiliko kiutawala na kiutendaji ikilinganishwa na miaka ya zamani.
“Hii shule ni kongwe nchini, ina zaidi ya miaka 30, tunajua hali ilivyokuwa kuanzia majengo hadi kitaaluma ila kwa sasa tunaona maendeleo yaliyopo, kikubwa ni viongozi wa juu kuiona kwa jicho la tatu,” amesema Mangi.
Akielezea hatua wanazochukua, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mbeya, Abdul Komba amesema watakaa Kamati ya Utendaji ya Chama Wilaya kisha kuwasilisha ripoti ili kuona juhudi hizo zinafanikiwa.
“Tunapongeza kazi nzuri ya bodi na sisi tutakaa haraka kuhakikisha hizi juhudi zinaungwa mkono na chama kwa kuwa shule inafanya vizuri kitaaluma, naamini viongozi wa juu watafika hapa kuona, niwaombe viongozi, wadau waliosoma hapa watupe nguvu,” amesema Komba.