Siri mafundi simu kuhusishwa katika uhalifu

Dar es Salaam. Kutokana na maendeleo ya teknolojia, simu za mkononi sasa ni zaidi ya kifaa cha mawasiliano.

Simu zimekuwa zikitumiwa kama chanzo cha kujipatia kipato katika biashara na kuhifadhi taarifa binafsi, zikiwamo za siri.

Mbali ya hayo, zinachangia katika mnyororo wa ajira wakiwamo za wauzaji simu, vifaa vyake na mafundi wa kuzifanyia matengenezo zinapopata hitilafu.

Katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, kama yalivyo maeneo mengine,  wamekuwapo wauzaji wa simu na vifaa vyake, pia mafundi; mitaa ya Uhuru, Msimbazi, Likoma, Aggrey, Magila na Muhonda ikiwa mahususi kwa shughuli hizo.

Wanapotekeleza majukumu yao, mafundi huwa na fursa ya kuzifikia data na taarifa nyeti kutoka kwenye simu za wateja.

Ni kutokana na namna mafundi wanavyozitunza au kuzitumia data na taarifa hizo, hujikuta wakiingia kwenye matatizo, yakiwamo ya uhalifu.

Si hivyo tu, baadhi ya mafundi wanatuhumiwa kutumia ofisi zao kuficha kazi nyingine wafanyazo, baadhi zikifanyika kinyume cha sheria.

Ili kuitambua rasmi kazi ya ufundi simu, mwaka 2020 Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Daffa alisema wanaweka utaratibu wa mafundi simu kusomea taaluma hiyo ili wapate leseni.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini wapo mafundi simu ambao hawana taaluma wala leseni ya kufanya kazi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Desemba 31, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari alisema mafundi wanaofanya kazi kinyume cha sheria wanachukuliwa ni wahalifu, maana wao wanashughulika na aliyeomba leseni.

“Kama mtu anafanya shughuli hizo bila leseni ni kosa ni sawasawa na kufanya biashara bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na lazima kuchukuliwa hatua,” amesema.

Amesema mamlaka ipo kusimamia sekta nzima ya mawasiliano na kuchukua hatua kwa kila kosa kulingana na namna lilivyotokea na inafanya hivyo kwa nchi nzima na si kwa kulenga mahali fulani.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini wapo mafundi simu wanaojihusisha na biashara za uuzaji simu zilizoibwa ambazo mbali na kufutwa taarifa zilizomo, hubadilishwa namba za utambulisho wa simu (IMEI).

Amir Hussein (si jina halisi), mmoja wa mafundi simu, anasema biashara ya vuifaa hivyo hufanyika kwa usiri, hali inayowafanya baadhi ya mafundi kuwa kwenye hatari ya kukamatwa kwa uhalifu.

“Katika mkusanyiko wa watu wengi kila mmoja ana jambo analofanya. Siku hizi kumeibuka wimbi la vijana ambao wamejikita katika utengenezaji wa simu,” anasema fundi huyo anayefanya shughuli zake Kariakoo.

Anasema kwa kiasi kikubwa maduka hufungwa saa 12:00 jioni lakini baadhi ya mafundi simu huendelea na kazi kwa maelezo kuna wateja muhimu.

“Tunapofunga maduka jioni, kuna mikutano ya siri hufanyika, watu wanauziana simu na vifaa vingine, zipo pia simu mpya zilizotoka kwenye maduka mengine au zile zilizoporwa mitaani,” anasema.

Anaeleza upo mtandao unaopokea simu za wizi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, kazi ya mafundi ni kuzifanyia marekebisho ya namba za IMEI ili zionekane mpya na kuziuza.

“Biashara hii inalipa lakini ni hatari sana, kuna wakati wateja wanarudi na kusema simu zao zimeshikwa na polisi au maofisa wa usalama.

“Wengine wameripoti kufuatwa na watu wasiojulikana ambao wanataka kujua jinsi walivyopata simu wanazozitumia,” amesema.

Anasema mafundi pia hupokea simu na vifaa vyake kutoka kwa makuli au wasaidizi wa kwenye maduka ambao huvipeleka Kariakoo.

“Kuna baadhi ya vifaa tunauza tunavitoa kwa watu ambao wanafanya kazi kwenye maduka makubwa yakiwepo yale ya mjini ambao wanaingiza mizigo mikubwa, wakileta huku tunawapa pesa kidogo,” anasema.

Anasema kutokana na biashara hiyo, wamekuwa wakikutana na watu wasiowajua.

Anakiri baadhi ya mafundi wamekuwa wakikamatwa na Polisi na watu wengine wasiojulikana.

Anaeleza mara nyingi wanaowachukua mafundi simu hawavai sare za polisi, hivyo kutotambua kinachoendelea.

Fundi mwingine, Juma Ramadhani amedai wamekuwa wanawaogopa mafundi wenzao katika eneo hilo lakini wamekuwa na mafanikio ya ghafla.

Anasema mafundi hao wameanza kazi muda mfupi lakini wana mafanikio ya haraka, tofauti na walio kwenye fani kitambo.

“Sisi wenyewe huwa tunajiuliza mtu amekuja siku chache lakini ndani ya miezi mitatu au minne ameshakuwa na pikipiki au gari, wakati mimi nipo hapa mwaka wa nane nafanya kazi hizi sijawahi kuwa na mafanikio ya hivyo,” anasema Juma.

Anasema cha kushangaza huwa wanafungua fremu (maduka) za gharama bila kuchangia na mtu na baada ya muda wanasikia ameanza safari za nje ya nchi.

Halima Mwinyijuma, mteja ambaye mara kadhaa amekuwa akitengeneza simu Kariakoo anasema aliwahi kushuhudia fundi aliyekuwa akimtengenezea simu akichukuliwa na watu baada ya mazungumzo ya muda mfupi.

“Nikiwa kwa fundi mtaa wa Likoma walikuja watu watatu wakatusalimia, wakamuita fundi, sikuelewa kilichoendelea kwa sababu hakusema kitu zaidi ya kunikabidhi kwa fundi mwingine,” anasema Halima.

Uvujishaji siri za wateja

Baadhi ya mafundi wamekuwa wakihusishwa na shughuli zisizo na maadili, ikiwemo kuvujisha siri za wateja na kufuatilia mahusiano ya watu.

“Mafundi tuna tabia tofauti, wakati mwingine tunajiuliza kwa nini haya yanatokea kwa wenzetu, tukifuatilia tunakutana na kesi ambazo ziliwalenga kwenye tamaa,” anasema Shaban Kilago.

Inaelezwa baadhi ya mafundi simu hufanya kazi ya kufuatilia mahusiano ya watu.

Kwa mujibu wa Kilago, mafundi huingiza programu kwenye simu za walengwa ambazo zinaruhusu wenza kupata taarifa kuhusu mazungumzo, picha na maeneo watakayokuwepo muda wote.

“Biashara hii imekuwa na matokeo mabaya kwa kuwa na matukio yaliyosababisha migogoro ya familia, kuvunjika kwa ndoa, vurugu kutokana na wivu au hasira kwa kuchochewa na ufuatiliaji,” anasema.

Mbali ya hayo, anasema wapo wateja wanaofika na simu zilizohusika kwenye matukio wakitaka kila kitu kiondolewe zikiwamo picha na mawasiliano. Wengi wa aina hiyo, anasema hudai simu wamepewa na ndugu zao.

Kilago anasema wameanza kushtuka kununua simu za mkononi baada ya Jeshi la Polisi kuwafuatilia pindi simu zinapoibwa katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam.

Mweneyekiti wa chama cha mafundi simu, Ahmada Ramadhani ameieleza Mwananchi Januari 2, 2025 kuwa yanayotokea ni tabia ya mtu na si mafundi simu wote wanafanya uhalifu.

Amesema inapotokea mtu anakamatwa ahusishwe yeye na si tasnia nzima ya ufundi.

“Simu ndiyo inayochochea uhalifu na si fundi kwa sababu hakuna sehemu kwenye taaluma wanafundishwa uhalifu, hivyo Jeshi la Polisi wanatakiwa kukaa ili tuwaelezee changamoto zetu na si kuitwa kuwa wasikilizaji,” anasema.

Anasema wapo watu wanaiba simu na kuzipeleka kwao kutengeneza, si rahisi wao kutambua kama ni ya wizi ila ana uwezo wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kumpata muhusika kutokana na utaalamu walionao.

Ahamada anasema kuna biashara haramu za simu ambazo polisi wanatakiwa kufahamu zinapelekwa wapi na masoko yako wapi, akieleza wangedhibiti huko ingekuwa rahisi kwa sababu wao wanadili na wamiliki wa simu.

“Asilimia kubwa ya mafundi simu wanaokamatwa kesi zinakuwa si za kwao bali za kuangukiwa zilizotokana na simu walizoletewa,” anasema.

Anasema baadhi ya mafundi simu wanatumia ofisi zao kufanya uhalifu na sheria ikimtia hatiani anapaswa kuhukumiwa, kwani tangu chama chao kiliposajiliwa mwaka 2008 wamekuwa wakieleza miiko ya kazi zao.

Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao Makao Makuu Jeshi la Polisi, Joshua Mwangasa akizungumza na Mwananchi Desemba 29, 2024 alisema wanaangalia sheria za nchi, ikiwemo ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 zinasema nini katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

Anasema operesheni nyingi zinafanyika kwa mafundi simu, akieleza wamewahi na wanaendelea kufanya programu za pamoja za mafundi simu waliosajiliwa na TCRA.

“Mafundi simu wamekuwa sehemu ya intelijensia yetu kwa kuwaeleza kuwa wanapoona mtu anakuja na kifaa ambacho wanahisi ni cha wizi basi wao wanashirikiana kutupa taarifa,” anasema.

Anasema kuna mbinu nyingine hawawezi kuweka wazi lakini wanashirikiana na mafundi simu na viongozi wao.

Mwangasa amesema wamekuwa wakitoa elimu ya namna ya kujilinda katika uhalifu wa kimtandao kwa kuamini kuwa, kwa kumjengea mwananchi uelewa watapunguza uhalifu wa kimtandao kwa asilimia kubwa.

“Suala la fundi simu hawezi kukulazimisha bali inakuwa makubaliano ya kuhitaji huduma na yeye anaweza kuwa na mambo yake kwa sababu si kila mtu ni mwaminifu, cha msingi mwenye kifaa kabla ya kupeleka kwa fundi aangalie kama kuna mambo nyeti aweze kuondoa,” amesema.

Related Posts