Tanga. Mkandarasi anayetekeleza sehemu ya tatu ya barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange, Pangani, Tanga yenye urefu wa kilomita 95.2, amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Waziri wa Ujenzi, Abdalla Ulega alipomtaka aeleze sababu za kusuasua kwa ujenzi huo.
Hata hivyo, katika utetezi wake kwenye utekelezaji wa mradi wenye thamani ya Sh111.55 bilioni, mkandarasi huyo kutoka kampuni ya M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation (hakutaka kutaja jina lake), amemweleza Waziri Ulega sababu mbalimbali ikiwemo mvua za mara kwa mara zinazosababisha kusuasua kwa ujenzi huo.
Njia hiyo ni sehemu ya barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ipo kwenye ushoroba wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi – Mombasa Lunga Lunga, Kenya na Horohoro na Tanga – Pangani – Bagamoyo, Tanzania wenye urefu wa jumla ya kilometa 454.
Waziri Ulega amembana mkandarasi Januari 2, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo miradi ya barabara ya Tanga – Pangani na daraja la Pangani.
Katika ziara hiyo, Waziri Ulega aliambatana na viongozi waandamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), pamoja na Mtendaji Mkuu, Mohamed Besta na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Baltida Burian.
Licha ya kutoa sababu hizo, Waziri Ulega hakukubaliana na suala hilo, aliagiza Tanroads kumuandalia ripoti kuhusu ujenzi huo na mapendekezo na hatua za kushauri ili mchakato huo upate suluhisho, akisisitiza maelezo yaliyotolewa na mkandarasi hayawezi kueleweka kwa wananchi.
“Mvua ni za Mungu, sisi tumekupa kazi wewe mtalaamu na unajua kwamba kuna siku itanyesha na siku nyingine jua litawaka. Haiwezekani mradi uwe umebakisha miezi mitatu uwe asilimia 40, halafu utuambie kuna tatizo la mvua nyingi,” amesema.
Kwa mujibu wa Ulega, mwenendo wa mtiririko wa fedha kwenda kwa mkandarasi huyo, amebaini hawaidai fedha nyingi Serikali za kushindwa kutimiza majukumu yake hayo kwa wakati.
“Hawa wanaojenga daraja hili wamefikia hatua nzuri na wapo kwenye maji, ila wewe ulitakiwa ufikie asilimia 90 ila upo asimilia 40 tu.
“Watanzania wanasubiri barabara ya Afrika Mashariki ikamilike sababu za namna hii, haziwezi zikaelezwa kwa wananchi zikaeleweka,” amesema Waziri Ulega.
Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema barabara hiyo ina awamu tatu; ya kwanza kutoka Tanga hadi Pangani, kilomita 50, pili ujenzi wa daraja na tatu Pangani hadi Makurunge mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani alimuomba Waziri Ulega kuhakikisha mkandarasi anayejenga barabara ya Tanga hadi Pangani anaikamilisha kwa wakati ili kuondoa kero kwa wananchi.
Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu alimuomba mkandarasi anayetekeleza mradi wa Tanga – Pangani kukamilisha kwa wakati akisema ni njia muhimu katika kukuza uchumi.
Endapo barabara hiyo itakamilika itachochea ukuaji wa uchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kurahisisha usafirishaji kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa nchini Kenya.
Pia, kutachochea uchumi wa buluu pamoja na kupunguza muda wa usafiri, urahisishaji wa kufanya biashara na kuwezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii.
Ataka vijana kupewa fursa
Katika hatua nyingine, Ulega amesema hajaridhika na idadi ya vijana wa Pangani wanaoshiriki ujenzi wa daraja la Mto Pangani litakalounganisha mikoa ya Tanga na Pwani kupitia barabara ya EAC.
“Mmeniambia wapo vijana wengi wanaofanya kazi hapa, maelekezo ya Serikali, hii miradi iwanufaishe vijana wenyeji wa maeneo husika. Sio lazima kazi zote za kitaalamu basi watoke maeneo mengine, ila wale vijana 304 mlionionyesha pale si kweli wanatoka Pangani wengi mmewachukua maeneo mengine,” amesema Ulega.
Hata hivyo, Ulega alielezwa kati ya 325 vijana 79 ndiyo wanaotoka Pangani wakiwemo vibarua na watalaamu.
Akijibu suala hilo, Msimamizi wa Mazingira na Uhusiano na Jamii kutoka kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Bazir Kisira amesema wafanyakazi 79 sawa asilimia 26.1 akisema kwa asili ya ujenzi huo unahitaji watalaamu wengi kuliko wasaidizi.
“Shughuli zote tunazozifanya zinazohitaji zinazohusisha wafanyakazi au watalaamu wa kati na juu na wasaidizi huwa tunawasiliana na serikali za vijiji ili kuwapa taarifa za kuhitaji watu na wakipatikana tunawatumia,” amesema.
Baada ya majibu hayo, Ulega amesema zipo kazi ambazo hazihitaji shahada ya chuo kikuu ikiwemo ubebaji akitaka watoe fursa zaidi kwa vijana wa Pangani kwenye mchakato huo, akiahidi kulifuatilia kwa umakini suala hilo.
Akizungumzia barabara ya Tanga – Pangani yenye kilomita 60, Ulega amesema kwa nyakati tofauti wabunge wamekuwa wakipaza sauti ikamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake wa kuufungua mkoa huo.
Kutokana na umuhimu huo, Waziri Ulega amesema Serikali ilitoa fedha Sh4.7 bilioni kwa mkandarasi Chico ili kurejesha vifaa, watalaamu na vibarua katika eneo la mradi ili kazi iendelee.
“Rais Samia Suluhu Hassan ni msikivu amedhalimia kuboresha miundombinu, sio hapa Tanga bali katika mikoa mingine,” amesema Waziri Ulega.