Moshi. Ni kukua kwa teknolojia ya mawasiliano ya habari, ulimbukeni au malezi mabaya? Ni maswali yanayoumiza wengi kwa sasa, baada ya kuibuka wimbi la usambaaji picha za ngono, video na za mnato, kupitia mitandao ya kijamii.
Video hizo baadhi wanatajwa kujirekodi au kurekodiwa kwa hiyari na kuzisambaza wakiwamo wahitimu wa vyuo.
Kutokana na wimbi hilo kuhusisha wasichana wadogo na wanafunzi wenye umri kati ya miaka 20 na 25, wadau wa elimu, wanaharakati na wanasheria wametaja mambo manane yanayochangia hali hiyo.
Wadau hao wamezitaka mamlaka zinazosimamia makosa ya kimtandao kuhakikisha wanashughulikia hali hiyo, kwa kuwa sheria ya uhalifu wa kimtandao inatoa adhabu ya faini ya hadi Sh20 milioni au kifungo miaka saba jela.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ubunifu katika Elimu (EIT), Benjamin Nkonya amesema kutokana na uhaba wa wasichana wa kazi, wazazi wamejikuta wakiajiri wasio na maadili ambao hufanya michezo michafu na watoto wa kiume, kujirekodi na kurusha mitandaoni.
Mambo yanayojatwa na wadau kuwa kiini cha usambazaji wa picha hizo ni tatizo la ajira linalowasukuma baadhi ya wasichana kujiingiza katika ukahaba.
Mengine ni watoto na wanafunzi wanaonunuliwa simu janja na baadhi ya wazazi kutokuwa na elimu ya matumizi sahihi ya mitandao, saikolojia ya makundi, tatizo la afya ya akili na malezi mabaya.
Yanatajwa pia vijana kuingia katika uraibu wa ngono, ushamba na ulimbukeni wa mapenzi, wazazi na jamii kutotimiza kikamilifu majuteknolojia ya habari na mawasiliano kama kiini cha tatizo.
Akizungumza na Mwananchi Januari mosi, 2025, mwanazuoni na padri wa Kanisa Katoliki, Dk Aidan Msafiri amesema nguzo nne za malezi ziko mahututi na kizazi cha kuanzia mwaka 2000 maarufu Gen-Z kimegeuka mateka wa usasa hatarishi.
“Kimsingi kuna kizazi cha kisasa ambacho kimekosa malezi ya msingi katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni kwenye familia,” amesema Padri Msafiri anayefundisha vyuo vikuu ndani na nje ya nchi.
Amesema malezi ya upande mmoja ni tatizo, akieleza kinamama wengi ndio wanalea watoto au hulelewa na bibi au shangazi, hivyo kukosa malezi ya baba na mama.
“Nguzo nyingine ni shule. Shule zamani ilikuwa ni mahali pa malezi. Zilikuwa ndiyo zinamuonyesha mtoto hili ni jema fanya, hili ni baya usifanye. Shule nyingi sasa ni kukaririshwa tu masomo na mwalimu naye anafanana na mtoto,” amesema.
Amesema baadhi ya walimu hawana mamlaka na watoto: “Shule nyingi hivi sasa ni biashara, hakuna malezi, hakuna maadili. Walimu wanavaa vibaya, walimu na wao wanajionyesha kila kitu na kujipiga picha za ajabu ajabu. Unategemea mwanafunzi wake aige lipi jema?”
Sehemu ya tatu amesema ni dini, akieleza wengi leo hii hawapendi kuonywa na kuambiwa mambo ya ukweli, ndiyo maana wameingia katika dini ambazo hazina sheria.
“Kama vile timu ziingie uwanjani bila kanuni za mpira. Misingi ya maadili ya Kimungu imepigwa chini. Kwa hiyo dini hivi sasa imekuwa ni dili, ndiyo maana unaona kunaibuka dini nyingi lakini wanadamu hawabadiliki wala hawana hofu ya Mungu,” amesema.
Nguzo ya nne amesema ni jamii, akieleza baadhi ya wana jamii wamekuwa wa hovyo, hawajali kulea wala kulelewa.
“Tukijumlisha hizo nguzo zote nne ambazo ziko ICU, ndiyo tunapata kizazi hiki tulichonacho. Mtu aliyezaliwa kuanzia mwaka 2000 wengi ni shida. Unaweza kuita ni Gen-Z au kizazi cha kisasa. Ukimwambia kitu, lazima aanze kwa kupinga. Unamweleza kitu cha ukweli na cha manufaa kwake anakupinga tu,” amesema.
Amesema kuna mapinduzi ya uasi, akieleza baada ya kupinga kila kitu, ndipo hubaini alifanya kosa.
Wakili wa kujitegemea na kiongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Kaskazini, David Shillatu ametaka jamii na Serikali kuamka kutoka usingizi mzito kwa kuwa kizazi cha watoto wa sasa kinaangamia.
“Wakati ni huu, hatupaswi kuendelea kukaa kimya wakati sisi wenyewe, watoto wetu na au watoto wa watoto wetu wakidhalilishwa. Tunapaswa kuamka kabla hatujachelewa sana,” amesema.
Amesema mitandao ya kijamii ina masharti ya kipekee na wakati huohuo ina vipengele vya utashi wa mtumiaji.
“Masharti hayo yanaelezwa kwa lugha ndefu za Kiingereza na watumiaji bila kusoma kwa kina masharti yale huwa wanakubali kwa kuwa wanakuwa na mbio tu kuingia mle. Matokeo yake ndiyo haya tunayaona, tupu za watoto wetu wadogo kabisa na wengine ni watu wazima lakini ndiyo hivyo taarifa zao za faragha zinawekwa hadharani katika kiwango ambacho hatujawahi kukishuhudia,” amesema.
Amesema zipo sheria kali nchini zikiwamo Sheria ya Uhalifu Mtandaoni ya mwaka 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 ambazo kama zitasimamiwa vizuri, zinaweza kupunguza kama si kudhibiti kabisa wimbi hilo.
“Ili kukomesha vitendo hivi ni wajibu wa jamii ya Watanzania, vyombo vya habari vikiwa mstari wa mbele kuelimisha umma juu ya uwepo wa sheria hizi na namna gani waepuke kuingia matatizoni,” amesema.
Wakili Peter Mshikilwa wa jijini Dar es Salaam anasema kinachochangia hali hiyo ni kutokuwepo uelewa wa utumiaji wa mitandao na uwepo wa unyanyasaji wa kimtandao. Hata hivyo, amesema sheria zinaweza kuondoa kadhia hiyo.
Renalda Evance, mzazi na mkazi wa Kiborlon, Manispaa ya Moshi, ameitaka Serikali iingilie kati, wanaosambaza video hizo wakamatwe na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
“Vijana wetu wajifunze kuishi maisha ya kawaida. Sawa inawezekana hali ngumu ya kipato inasababisha binti kujirekodi ili apate wafuasi mitandaoni aweze kulipwa. Lakini maadili na sheria zinasemaje,” amehoji.
Emiliana Johnson, anayejishughulisha na uuzaji wa mbogamboga majumbani, amehoji inakuwaje anayekosoa Serikali mitandaoni anatafutwa kwa nguvu zote na kukamatwa lakini wanaosambaza video za ngono hawaguswi.
“Mtukane kiongozi yeyote wa Serikali sasa hivi mtandaoni kama utachukua wiki hujakamatwa, au siyo kosa kusambaza video za ngono? Tena utasikia naomba connection (video) na vyombo vyetu vya dola vipo,” amedai.
Mdau wa elimu, Wilfred Mauki ambaye ni mwalimu kitaaluma, amesema kizazi cha sasa cha wanafunzi, wengi wameshindwa kutumia simu janja kwa lengo la kupata maarifa shuleni na kujiingiza katika mambo yasiyofaa.
“Wanafunzi wengi wa kike na wa kiume wameweka mbele mambo ya kuiga yasiyokuwa na utamaduni wa Mtanzania, hii imesababishwa na kukosekana kwa somo la maadili mashuleni.
“Somo la dini likifundishwa kikamilifu mashuleni litawafanya wawe na hofu ya Mungu. Hapa lawama moja kwa moja inaenda kwa jamii kwani ndiyo imekuwa vinara wa kusambaza picha za video jambo ambalo siyo zuri kwa Taifa letu,” amesema.
Kwa upande wa shule amesema wanapaswa kuangalia mwenendo wa mwanafunzi na usimamizi makini wa nidhamu, huku Serikali ikiwa na wajibu wa kusimamia sheria zinazozuia usambazaji wa video hizo.
Nkonya wa EIT amasema tabia ya kusambaza picha za ngono mitandaoni ni matokeo ya urahisishaji wa mawasiliano ulioletwa na mifumo ya kimtandao na kuchagizwa na mfumo wa elimu wa Tanzania.
“Mfumo wa elimu unatoa wahitimu wa vyuo vikuu ambao hawawezi kumudu ushindani wa kimataifa wa soko la kazi zenye malipo mazuri ambazo zimegubikwa na utandawazi kama zabuni za Serikali,” amesema.
Amesema matokeo ya hali hiyo ni baadhi ya wahitimu wa kiume kufanya kazi zisizoendana na taaluma zao kama kuendesha bodaboda, umachinga au hata kujiingiza kwenye shughuli za aibu kama ushoga.
“Kwa wahitimu wa kike, kumezuka tabia ya baadhi yao kutumia sana mitandao ya kijamii kujitangaza ili waendeshe ukahaba wajipatie fedha za kujikimu mahitaji yao ya kila siku,” amesema.
Nkonya amesema kutokana na Serikali kuchukua wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kujiunga na sekondari, kumeibuka changamoto ya kupata wasichana wa kazi, hivyo baadhi ya wanaoajiriwa ni wale wenye tabia mbaya, walioshindikana ambao wamekuwa wakiwafundisha watoto wanaowalea masuala ya ngono.
Ameshauri wazazi wahamasishwe kuwadahili watoto wadogo katika vituo maalumu vya kulelea watoto wakati wa mchana kwa kuwa kuna udhibiti mkubwa wa Serikali katika masuala ya malezi.
“Lakini mfumo wa elimu urekebishwe ili wale wanaofadhiliwa na Serikali kusoma elimu ya juu wawe wale tu ambao soko la kazi hasa la ushindani, linawahitaji. Hii itawezekana pale tu wizara yenye dhamana na kazi ifanye utafiti kwa kuitumia HESLB (Bodi ya Mikopo) kulipia wale tu wanaohitajika kwenye soko la kazi za ushindani,” amesema.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Maadili Centre, Florentine Senya, amesema tatizo linaanzia pale vijana wanapopewa simu au kununua simu bila kuwa na elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yenye manufaa.
“Wazazi wanamkabidhi tu mtoto simu wala hawafuatilii anatazama nini. Kuna programu (application) wakati mtoto anapojiunga na Google inaweza kukuambia kila kitu mtoto anachoangalia au kupakua,” anasema.
Senya amesema wazazi wanawaacha watoto kama kuku wa kienyeji ambao huingia mitandaoni na kubeba kila wanachokuta bila udhibiti, huku kwenye makundi sogozi wakitumiana hadi video za ngono.
Mkurugenzi wa Shirika la KWIECO mkoani Kilimanjaro, Elizabeth Minde amelaani sambazaji wa video hizo akisema unaathiri malezi na makuzi ya mtoto.