Watatu kortini wakidaiwa kusafirisha kilo 1,500 za bangi

Dar es Salaam. Wakazi watatu jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi, yenye uzito wa kilo 1,501.

Katika kesi ya kwanza, Mohamed Bakari (40) na Suleshi Mhairo (36), wakazi wa Mabibo wamesomewa shtaka la kusafirisha kilo 1,350 za bangi.

Washtakiwa ambao ni wafanyabiashara wamefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa Januari 3, 2025 na kusomewa shtaka katika kesi ya uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali, Titus Aaron.

Wamesomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Kabla ya kusomewa mashtaka, hakimu Nyaki alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Pia, kiwango cha dawa wanachodaiwa kukutwa nacho hakina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Akiwasomea mashtaka, Wakili Aaron amedai Novemba 12, 2024, eneo la Nyakwale lililopo Kigamboni, Bakari na Mhairo wanadaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 1,350, wakijua ni kosa kisheria.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na umeiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Bakari alinyoosha mkono kuomba nafasi ya kuongea, aliporuhusiwa na hakimu Nyaki alikiri shtaka linalomkabili na sehemu ya maelezo yake ilikuwa kama ifuatavyo.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, mimi nakubali kosa.

Hakimu: Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu au ulikuwa hujanielewa? Mwanzo niliposema washtakiwa hamtakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hakimu: Wakikamilisha upelelezi upande wa mashtaka, mtapelekwa kwenye Mahakama inayosikiliza kesi yenu na huko ndipo utakapokiri shtaka lako.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, mimi pekee yangu ndiyo nina husika.

Hakimu: Nasema upelelezi ukikamilika, kesi hii itahamishiwa kwenye Mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi au kama Mahakama ya Kisutu itapewa mamlaka ya kusikiliza shauri hili, hapo sasa ndipo utakapokiri shtaka lako, umeeelewa?

Mshtakiwa: Kimya… huku akiendelea kuangalia kwa makini nakala ya hati ya mashtaka aliyopewa na upande wa mashtaka mahakamani hapo.

Hakimu Nyaki baada ya kutoa ufafanuzi aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 16, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Katika kesi ya pili mkazi wa Chanika Buyuni, Idd Mohamed Idd (46) amefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja la kusafirisha kilo 151.43 za bangi.

Idd ambaye ni dereva, amesomewa shtaka na Wakili wa Serikali Aaron, mbele ya hakimu Nyaki.

Upande wa mashtaka umedai mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 13, 2024 katika eneo la Pweza, Sinza E, lilolopo Wilaya ya Kinondoni.

Inadaiwa siku ya tukio, mshtakiwa alikutwa akijihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 151.43 kinyume cha sheria.

Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na mshtakiwa amerudishwa rumande kutoka na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Hakimu Nyaki ameahirisha kesi hadi Januari 16, 2025, itakapotajwa.

Related Posts