Watoto watatu wafa maji kwenye lambo

Siha. Watoto tatu wa familia moja wamefariki dunia katika Kijijii cha Ngaratati, Kata ya Makiwaru wilayani Siha walipokuwa wakiogelea kwenye lambo lilijengwa na Serikali kwa ajili ya mifugo kupata maji.

Diwani wa kata hiyo, Ezekiel Lukumai amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Januari 2, 2025 watoto hao walipokwenda kufua nguo na kuoga.

Amesema mmoja wa watoto hao ana miaka tisa na ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Ngaratati. Amesema wawili wenye miaka sita kila mmoja ni wanafunzi wa shule ya awali.

Amesema siku ya tukio watoto hao wa kike walikuwa na baba yao mzazi nyumbani. Mzazi alipoingia ndani kwenda kupumzika, wenyewe waliondoka kwenda kwenye lambo ambalo halipo mbali na nyumba wanayoishi kuoga na kufua nguo.

Ameeleza walipokuwa wakiogelea maji yaliwazidi wakafariki dunia. Lukumai amesema walipata taarifa za tukio hilo kutoka kwa watoto wengine waliofika eneo hilo.

Ameeleza baada ya kupata taarifa walipiga kelele kuomba msaada wa wananchi. Walipofika eneo la tukio walikuta karai na nguo zilizofuliwa pembeni mwa lambo.

Watoto hao walikutwa wakielea juu ya maji wakiwa wameshakufa. Amesema polisi walifika kuchukua miili ya watoto hao ambayo imehifadhiwa katika Hospitali ya Kibong’oto.

Ameshauri watoto wasiruhusiwe kupeleka mifugo eneo hilo kwani wamekuwa wakionekana kuogelea na pia pawekwe uzio ili kuwa na ulinzi wa kutosha.

Lukumai amesema lambo hilo lilipojengwa kulikuwa na uzio ambao uliharibiwa.

Julius Mollel, mkazi wa eneo hilo amesema upungufu wa maji kwenye mabomba unachangia baadhi ya watu kwenda kufua nguo kwenye lambo hilo.

“Maji kwa wiki yanakuja mara moja au mbili, hili ni tatizo linalosababisha watu kwenda kufua nguo kwenye eneo la lambo,” amesema.

Mwenyekiti wa kijijii hicho, Nurueli Kivuyo amesema watoto walikwenda kufua nguo na kuoga, akieleza hajui nini kiliwakuta na kukutwa sehemu moja wakiwa wamefariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema yupo nje ya ofisi, akiahidi kufuatilia taarifa za tukio hilo.

Related Posts