Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia wafanyabiashara wawili kwa tuhuma za kupatikana na miundombinu ya umeme na maji kinyume cha sheria.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Januari 3, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia msako uliofanywa maeneo ya Nzovwe, Uwanja wa Ndege wa zamani na Mtaa wa Block T.
Amesema msako huo ulihusisha maofisa wa Shirika la Umeme (Tanesco) wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wataalamu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya-Uwsa).
Kuzaga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Movin Joseph (53) mfanyabiashara wa vifaa vya umeme eneo la Block T na Rehema Jamson (42) mfanyabiashara wa vyuma chakavu katika eneo la Nzovwe jijini hapa.
“Operesheni hiyo maalumu tuliifanya kwa kushirikiana na maofisa wa Tanesco mikoa ya Nyanda za juu Kusini kufuatia kuibuka kwa wimbi la uhalifu wa miundombinu linalosababisha kuiingizia hasara Serikali na wananchi,” amesema Kuzaga.
Amesema, awali polisi walipekua ghala la mfanyabiashara, Movin Joseph (53) eneo la Block T na kubaini vifaa mbalimbali vya wizi ambavyo ni mali ya Tanesco zikiwepo nyaya za shaba na vifaa vya transifoma vilivyo funguliwa.
“Tumebaini vifaa vya aina mbalimbali vilivyo funguliwa kwenye miundombinu ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya na Tanesco ambavyo wafanyabiashara hao walificha na kuviuza kwa vificho,” amesema.
Kuzaga amesema operesheni hiyo imetokana na kuibuka kwa matukio ya wizi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali mkoani hapa na kuwa msako utaendelea ili kuwabaini wengine.
“Hatutawafumbia macho wahalifu au wafanyabiashara wanaonunua mali za wizi na kuingiza sokoni wakati wakijua ni kosa kisheria na kuchochea vitendo vya wizi wa miundombinu ya serikali,” amesema.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mbeya, Gilbert Kayange alitangaza dau la Sh1 milioni kwa watu watakaotoa taarifa na kuwabaini wezi wa dira za maji.
Hatua hiyo ya Kayange ilitokana na kuibuka kwa wimbi la wizi wa dira za maji, hali iliyosababisha usumbufu kwa wananchi kukosa huduma.