Wawili wafariki, 18 wajeruhiwa ajali ya ndege

California. Watu wawili wamefariki dunia huku wengine 18 wakijeruhiwa baada ya ndege ndogo aina ya Van’s RV-10 kugonga ghorofa la kitega uchumi jijini California nchini Marekani.

Ajali hiyo imetokea saa 8:09 mchana wa kuamkia leo Ijumaa Januari 3, 2025 baada ya ndege hiyo isiyo ya kibiashara, yenye uwezo wa kubeba watu wanne, kugonga jengo la ghorofa lililokuwa linatumika kutengenezea samani za ndani na nguo.

Jengo hilo linamilikiwa na kampuni ya utengenezaji wa samani za ndani katika kaunti ya Orange katika mji wa Fullerton nchini humo.

Tovuti ya BBC imeripoti kuwa idara ya polisi katika jiji hilo, imechapisha kwenye mtandao wa X kuwa watu 10 wamekimbizwa hospitalini kutokana na majeraha yaliyosababishwa na ajali hiyo, hata hivyo wanane kati yao waliruhusiwa muda mfupi baadaye.

“Ndege ya injini moja, aina ya Van’s RV-10, imeporomoka saa 8:15 mchana,” imesema Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Shirikisho (FAA) ikinukuliwa na BBC.

Hadi sasa, idara hiyo ya polisi, haijatoa taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ajali, haijulikani kama watu wawili waliokufa walikuwa wafanyakazi au abiria waliokuwa kwenye ndege.

Polisi, pia, wanahamasisha watu kutoka majengo yaliyo karibu na wanawaomba wananchi kuepuka maeneo ya tukio.

Mbunge Lou Correa ambaye anawakilisha kaunti ya Orange, takribani maili 25 (kilomita 40) kusini mwa Los Angeles, amesema kuwa: “Jengo lililogongwa ni kiwanda cha kutengeneza samani.”

Katika ujumbe wake kwenye X, Correa alisema: “watu 12 kati ya waathirika ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.”

Picha za angani za eneo la tukio zinaonyesha vipande vya ndege ndani ya jengo hilo na ajali hiyo ilisababisha moto ambao ulizimwa na wafanyakazi wa zimamoto.

Hata hivyo, picha za usalama zilizorekodiwa kutoka kwenye jengo lililokuwa upande wa pili wa barabara, zinaonyesha mlipuko mkubwa, kwa mujibu wa vyombo vya habari katika eneo hilo.

“Watu wanatetemeka kutokana na tukio hili.

“Ulikuwa ni mlipuko mkubwa, mtu mmoja akasema ‘Oh Mungu, jengo linawaka moto’,” alisema shuhuda wa tukio hilo, Mark Anderson.

Eneo ambalo ndege imeanguka liko karibu na Uwanja wa Ndege wa Fullerton, takribani kilometa 10 (maili 6) kutoka Disneyland.

IMEANDIKWA NA HELLEN MDINDA KWA MSAADA WA MASHIRIKA.

Related Posts